CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeendela kuvuna wanachama wapya kutoka katika vyama vya upinzani, hali ambayo inaongeza idadi ya wanachama katika chama hicho ambao ni jeshi na moja ya karata muhimu katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla akiwa katika ziara yake wilayani Dodoma Mjini mkoani Dodoma amepokea wanachama wapya 280 kutoka katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA).
Makalla amesema wanachama hao wamekwazika kutokana na uamuzi wa chama hicho kuamua kupumzika na kutokushiriki uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyia Oktoba mwaka huu.
“Leo nyie ni mashahidinnimepokea wanachadema 280 kuja katika Chama Cha Mapinduzi, nimepokea kadi hadi mikono inauma leo ni kama kusema hapa Dodoma Mjini Chadema kwaheri, Wanahama kwa sababu viongozi wao wamefanya uamuzi ambao haukuwafurahisha,” amesema Makalla.
Ameongeza wanachama wao wanajua wanatakiwa kushiri uchaguzi kila baada ya miaka mitano na uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi umewapa hasira wananchi na kuamua kuhamia CCM.
Makalla ameutaka uongozi wa chama katika ngazi ya wilaya na Mkoa kuhakikisha wanachama hao wanapewa kadi ili kukamilisha uanachama wao katika chama hicho.