Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule ameeleza kuwa kutokana na kuimarika kwa huduma za afya ikiwemo ongezeko la Madaktari,Vifaa,Dawa pamoja na ufuatiliaji hasa katika huduma za kujifungua Mkoa wa Dodoma umeendelea kupunguza vifo vya kina Mama kutoka vifo 81 hadi 52.
Senyamule ameyaeleza hayo leo hii Jijini Dodoma Juni 25,2025 wakati wa Uzinduzi wa jengo la kupumzikia wagonjwa na wanaosubiria wagonjwa wao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma lililojengwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini Mhe Anthony Mavunde.
Na kuongeza kuwa miaka ya hapo nyuma uwezo wa vifaa vya Hospitali hii ulikuwa mdogo sana lakini hivi sasa madaktari bingwa wapo wa kutosha ambapo inaonesha dhamira ya Dkt Samia katika kuimarisha Sekta hii na kufanya rufaa ya Hospitali hii kudhihirika katika kutibu magonjwa mbalimbali ikiwemo mifupa,watoto na mengineyo ya kibingwa.
“Kutokana na kuimarika kwa huduma za kujifungua Mkoa wa Dodoma umeendelea kupunguza vifo vya kina Mama wanapojifungua kutoka vifo 81 hadi kufikia vifo 52, kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali yetu kwa kuongeza Madaktari,Vifaa,Dawa,Ufuatiliaji pamoja mambo mengine”.
Aidha amesema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa hakuna malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya huduma wanazopata Hospitalini hapo ambapo ni tofauti na hapo awali, kitu ambacho ameupongeza uongozi wa Hospitali hiyo kwa kusimamia utoaji wa huduma bora na kwa wakati.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini Mhe Anthony Peter Mavunde ametumia wasaa huu kutoa Rai kwa watumiaji wote wa jengo hilo jipya na la kisasa kuhakikisha wanakuwa walinzi wa kwanza na kulitunza ili lisipate uharibifu wowote kwani litahudumia vizazi na vizazi.
Sambamba na kuwaomba wadau wengine kujitokeza ili kuunga mkono jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuboresha Sekta ya afya kwani bado yapo maeneo mengi yenye uhitaji kama huu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
“Nitoe Rai kwa watumiaji wote wa jengo hili kwa kuhakikisha wanakuwa walinzi wa kwanza kwa kulinda na kulitunza jengo hili ili lisipate uharibifu wowote kwani litahudumia vizazi na vizazi”.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mwinyikombo Amir amesema kuwa mpaka sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma imeweza kulea Hospitali 10 zinazolingana hadhi na Hospitali hii katika masuala mazima ya ubingwa wa mifupa na mambo mengine ambapo moja kati ya Hospitali hizo ni Hospitali inayoongozwa na Shirika la Dini ikiwa ni katika kuhakikisha huduma za afya hazichagui na zinawafikia Watanzania wote.
Gharama za jengo hili,Vifaa pamoja Uzio uliowekwa umegharimu zaidi ya Milioni 40.