-Nishati safi ya kupikia ni endelevu
-Yaelezwa ni salama na mkombozi wa mazingira
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameacha alama mkoani Arusha kwa kugawa mitungi ya gesi 528 na majiko yake kwa watumishi wa jeshi la magereza mkoani ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama nchini.
Hayo yamebainishwa leo Juni 25, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu wakati wa uzinduzi wa kugawa majiko ya gesi kwa watumishi wa magereza iliyofanyika gereza kuu mkoani Arusha.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye kinara wa nishati safi ya kupikia nchini ambaye anaendelea kuhamasisha taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi na salama,” Amesema.
Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kuhamasisha na kuwataka watanzania wote kuhakikisha wanatumia nishati safi ya kupikia kama njia mahususi ya kutunza na kulinda mazingira na pia kuokoa uharibifu wa misitu
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewaeleza watumishi wa magereza kuwa nishati safi ni salama kwa Taifa kwa kuwa inaondoa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati isiyo safi na salama ya kuni na mkaa
“Ndugu zangu watumishi wenzangu, nawasihi sana kutumia nishati safi na salama katika matumizi yenu kwa sababu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka fedha nyingi ili kila mtanzania atumie nishati safi ya kupikia kuliko kutumia kuni na mkaa,” Ameongeza Mha. Saidy.
Akizungumzia kuhusu Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati safi ya kupikia ameeleza kuwa, lengo kuu la mkakati huo ni kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na malengo mengine mahususi ni kuandaa na kutekeleza kampeni maalum za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Magereza mkoa wa Arusha, ACP Prosper Kapinga ameipongeza REA kwa tukio hilo muhimu la kugawa mtungi wa gesi na majiko ya sahani mbili na kusema kuwa inaonesha kwa vitendo juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia Nishati Safi ya Kupikia.