-Kiwanda cha Shengde chakaribia kuanza uzalishaji rasmi mwezi Julai
Mkoa wa Dodoma unajiandaa kuandika historia mpya katika sekta ya usafishaji wa madini, kufuatia hatua za mwisho za ujenzi wa kiwanda kipya cha Shengde Precious Metal Resources Company Ltd, kilichopo eneo la Nala, ambacho kinatarajiwa kuanza rasmi uzalishaji wa copper cathode mwezi Julai, 2025.
Katika ziara maalum ya ukaguzi, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Menard Msengi, amesema ujenzi wa kiwanda hicho ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa agizo la Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, la kuhakikisha kuwa hadi kufikia Julai 30, 2025, usafishaji wa shaba yote inayochimbwa nchini unafanyika ndani ya mipaka ya Tanzania.
“Ujio wa kiwanda hiki ni kichocheo muhimu katika maendeleo ya Sekta ya Madini mkoani Dodoma na nchini kwa ujumla,” amesema Mhandisi Msengi, na kuongeza kuwa, “mradi huu utawanufaisha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia soko la uhakika, kuongeza thamani ya madini na kuongeza mapato ya wananchi pamoja na taifa.”
Kiwanda hicho ni miongoni mwa miradi inayofuatiliwa kupitia mradi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), unaolenga kuchochea maendeleo ya Sekta ya Madini ya viwandani, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa masuala ya mirabaha, usalama migodini na mchango wa sekta hiyo katika maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha Shengde, Abia Mafie, amesema tayari kiwanda kimeanza majaribio ya uzalishaji na kinaweza kuzalisha tani 20 za copper cathode kwa siku.
“Tunatarajia kuwasili kwa mitambo mikubwa zaidi itakayoongeza uwezo wetu hadi kuzalisha tani 1,000 kwa siku. Hii itawasaidia wachimbaji wadogo wenye changamoto ya kukosa soko kwa sababu ya viwango vya kimataifa,” ameeleza Mafie.
Akiwaonesha wageni jinsi uzalishaji unavyofanyika, Mafie amebainisha kuwa kiwanda hicho kinatumia kila kipande cha madini kilichopo: “Hata vumbi la copper tunalitumia kutengeneza tofali – hakuna kinachoachwa.”
Aidha, ametangaza mpango wa kampuni hiyo kujenga viwanda vingine vitano katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kama sehemu ya mchango wao katika jitihada za Serikali za kuongeza thamani ya madini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.