WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa onyo kwa wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya kwamba Tanzania siyo mahali pa kufanyia biashara zao.
Waziri Mkuu ambaye amefunga maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema: “Tanzania siyo mahali salama kwa wauzaji, wasafirishaji, walimaji na hata pia watumiaji wa dawa za kulevya. Tanzania tumeiva na sasa tunaenda kukomesha biashara hii.”
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Alhamisi, Juni 26, 2025) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Dodoma wakiwemo wananchi, wadau, viongozi wa Serikali, wa dini na siasa ambao walihudhuria kilele cha maadhimisho hayo kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
“Makamishna na wakuu wa vyombo vya ulinzi fanyeni kazi, imarisheni ulinzi iwe ni kwenye SGR, vituo vya mabasi, bandari na viwanja vya ndege ili tuweze kuokoa vijana wetu. Dawa hizi zina madhara makubwa kwani zinapoteza uwezo wa mwili na uwezo wa kiakili wa kufikiri mambo,” amesisitiza.
Amesema kuwa anatambua kwamba kuna mjadala ulioibuka baina ya wachumi na wadau wa kuzuia matumizi ya dawa za kulevya huku wachumi wakidai kuwa zinaleta fedha na kuacha kuangalia madhara ya kiafya ambayo wadau wanayasemea. “Kama tunataka tuwe na kundi la vijana wa Kitanzania mazezeta, basi turuhusu hii biashara. Lakini, Serikali hii tumekataa kwa sababu tunaamini kuwa hiyo mijadala haina tija na hatutairuhusu,” amesisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa.
Amesema kazi kubwa ya uwekezaji kwenye eneo hilo imefanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameongeza bajeti ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na kuwapatia vyombo vya usafiri ili wafanye kazi yao kwa ufanisi zaidi.
Akielezea kuhusu ugumu uliokuwepo wa kuhitimisha kesi za watu waliokuwa wanakutwa na dawa hizo, Waziri Mkuu amesema: “Lazima tulipongeze Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu Sheria ya Dawa za Kulevya itungwe; na hii ilikuwa ni baada ya kubaini kulikuwa na mapungufu kwenye mfumo wetu wa sheria,” amesema.
Aliwaeleza washiriki wa maadhimisho hayo kwamba kutokana na uwepo wa sheria hiyo, katika kila kesi 100 zinazofikishwa mahakamani, Serikali imeweza kushinda kesi 76.
Amesema ufanisi mkubwa unaoonekana hivi sasa unatokana na kufungamanishwa kwa Mamlaka ya DCEA ya Tanzania Bara na ile ya ZDCEA ya Zanzibar ambazo zinafanya kazi kwa karibu. “Kwa hiyo
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Naibu Waziri wa Nchi (OWM – Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderianga alisema Rais Samia ameweka fedha nyingi na vifaa ili kuhakikisha anawaokoa vijana wa Kitanzania kutoka kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imeongeza operesheni na usimamizi kwa kufungua ofisi za kanda ambapo mkoa wa Dodoma tayari unayo ofisi ya Kanda.
Naye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alisema kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kimataifa Tanzania iko vizuri. “Tunakotokea siyo hapa tulipo leo. Wakati ule, tulikuwa tunajulikana kama mapito ya dawa za kulevya. Lakini chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania tumeondoka kwenye doa hilo.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo alisema kutokana na uongozi madhubuti wa Serikali ya awamu ya sita, kwa kipindi cha kuanzia Juni, 2024 hadi Mei, 2025, kumekuwa na ongezeko la ukamataji wa dawa za kulevya ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Katika kipindi hiki, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, tumekamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu 2,301,414.94. Kiasi hiki ni kikubwa ikilingalishwa na kilo 2,050,542.73 zilizokamatwa kati ya Juni, 2023 na Mei, 2024. Kuanzia Januari hadi Desemba 2024, jumla ya kilo 2,327,983.8 zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 1,965,341 zilizokamatwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2023.”