Mwasisi wa chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Halima Sharif akisoma tamko la TAMWA juu ya kulaani udhalilishaji wa Wanawake katika mitandao ya Kijamii pamoja na kusisitiza heshima na hoja kwa viongozi wakike. Tamko hilo amelisoma katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa TAMWA unaofanyika leo Juni 27,28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania(TAMWA)Dkt. Rose Reuben akizungumza katika mkutano mkuu wa TAMWA unaofanyika leo juni 27, 28, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe akizungumza katika mkutano mkuu wa TAMWA unaofanyika leo juni 27, 28, 2025 jijini Dar es Salaam.
Mwanachama wa TAMWA, Betty Mkwasa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 27, 2025 baada ya mapumziko ya mkutano mkuu wa TAMWA. Ameeleza namna TAMWA ilivyomsaidia katika kukomboa wasichana na wanawake waliokuwa wakikabiliwa cha changamoto za ukatili wa kijinsi.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetoa tamko kali dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa wanawake, hasa viongozi wa kisiasa, vinavyofanyika kupitia mitandao ya kijamii kwa kutumia lugha chafu, dhihaka na matusi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwasisi wa TAMWA, Halima Sharif, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa chama hicho chenye wanachama zaidi ya 200 waliokusanyika na wengine kujiunga kwa njia ya ‘Zoom’ wakitafakari mafanikio, changamoto na fursa za chama hicho chenye historia ya miaka 39 ya utetezi wa haki za wanawake, watoto na makundi yenye uhitaji maalum.
Halima amesema vitendo vya udhalilishaji wa wanawake ni ukiukwaji wa maadili ya Kitanzania na vinahujumu jitihada za kujenga demokrasia jumuishi. “Mwanamke anapaswa kuhukumiwa kwa misimamo na hoja zake za kisera, siyo kwa jinsia yake wala sura yake,” amesema kwa msisitizo.
Ameeleza kuwa mitandao ya kijamii, licha ya kuwa chombo chenye fursa nyingi za mawasiliano na ushiriki wa wanawake katika mijadala ya kijamii na kisiasa, imegeuzwa na baadhi ya watu kuwa jukwaa la mashambulizi ya kisaikolojia dhidi ya wanawake, jambo ambalo linawakwamisha wengi kushiriki kikamilifu kwenye siasa na nafasi za maamuzi.
“Udhalilishaji huu wa mitandaoni ni kikwazo kwa demokrasia jumuishi na ni kinyume cha maadili ya Kitanzania,” ameongeza Halima.
Aidha, TAMWA imepongeza uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha kwa vitendo kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa mafanikio makubwa. Halima amesema kuwa Rais Samia ni mfano wa uthubutu, uzalendo, na maadili mema ya kiuongozi, na kwamba ameibua ari na imani kwa wanawake wengi kujiamini kushiriki katika uongozi wa taifa.
“Wanawake walioko kwenye nafasi za uongozi wanapaswa kuwa mfano kwa wengine, wakitambua kuwa wao ni kioo cha jamii na dira kwa vizazi vijavyo. Kufanya kazi kwa weledi na maadili ni njia bora ya kuvunja mitazamo potofu na kuimarisha imani kwa wanawake katika uongozi,” ameongeza.
Pia ameeleza dhamira ya TAMWA katika kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mazingira ya kazi, hususan kwenye vyombo vya habari, yanakuwa salama na jumuishi kwa wanawake.
Halima amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa sera za jinsia mahali pa kazi kama sehemu ya kuimarisha usawa wa kijinsia na kulinda utu wa wanawake.
Katika wito wake kwa jamii, Halima amesema, “Wanawake wanaweza, wanawake wanapaswa, na wanawake wataendelea kuongoza, kwa heshima, utu na hoja.”
Kwa zaidi ya miaka 39, TAMWA imekuwa chombo muhimu cha kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia, kuhamasisha sera na sheria za usawa wa kijinsia, pamoja na kuwajengea uwezo wanahabari nchini kufahamu kwa kina masuala ya jinsia, afya ya uzazi, ushiriki wa wanawake katika siasa, rushwa ya ngono katika vyombo vya habari, usalama wa kitaaluma, na matumizi ya TEHAMA katika kazi za habari.
Kwa kikao hicho TAMWA inarejelea upya dhamira yake ya kuendelea kuwa nguzo ya utetezi, uwezeshaji na uhamasishaji wa jamii juu ya haki, usawa na heshima kwa wanawake na makundi yenye uhitaji maalum.