Na Mwandishi Wetu, Moshi
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Enock Koola (35), ambaye aliongoza katika kura za maoni katika kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2020, amechukua tena fomu ya kuwania tena nafasi hiyo ya uwakilishi, akiwa miongoni mwa waliojitokeza kumkabili mbunge anayemaliza muda wake Dkt. Charles Kimei.
Mapema leo Juni 28, 2025 saa 2 asubuhi, katika siku ya kwanza ya uchukuaji fomu za kuomba kuteuliwa na (CCM) kugombea ubunge, katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Koola alikuwa mtia nia wa kwanza kufika katika Ofisi za CCM Wilaya ya Moshi na chukua fomu na kufuatiwa na washindani wengine watano, akiwamo Dkt. Kimei.
Wagombea wengine waliochukua fomu ni kuzirejesha leo kwa nyakati tofauti ni pamoja na Yuvenal Shirima, Diddas Lyamuya, Obrey Silayo na Lucy Mrema.
Baada ya kuchukua fomu katika Ofisi ya Katibu wa CCM, Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu kila mmoja kwa wakati wake, wagombea hao hawakuzungumza chochote na waandishi wa habari, badala yake kila mmoja alitoka na kwenda moja kwenye gari lake, kisha kuondoka.
Kivutio kikubwa katika uchukuaji na urejeshaji huo wa fomu walikuwa ni Koola na Dkt. Kimei, kutokana na ushindani mkubwa uliokuwapo baina yao katika kinyang’anyro cha mwaka 2020.
Itakumbukwa mwaka 2020 katika mchakato wa ndani wa chama, Koola ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi, alipata ushindi mbele ya wagombea wengine akiwamo Dkt. Charles Kimei ambaye ndiye aliyeteuliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho, kisha kushinda nafasi hiyo.
Koola ambaye ni msomi wa shahada ya uzamili (masters) alipata kura 187 kati ya 567 zilizopigwa, dhidi Dkt Kimei (ambaye alikuwa mshindani wake wa karibu) aliyepata kura 178 na kushika na nafasi ya pili. Wgombea wengine na kura zao kwenye mabano walikuwa Crisipin Meela (47), Laurance Mrack (44) na Regina Chonjo aliyepata kura 35.
Koola ni nani?
Katika siasa na uongozi, Enock mjumbe wa Baraza na mjumbe wa Kamati Utekelezaji wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM ya mkoa wa Kilimanjaro (2022 – 2027) na pia Mjumbe wa Baraza hilo katika Wilaya Moshi Vijijini (2022 – 2027).
Kielimu, Enock ni msomi ambaye amepata elimu katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo Mei 2022 alipata cheti cha kuhitimu mafunzo ya Uongozi wa Bodi kutoka Institute of Directors Tanzania (IoDT), Dar es Salaam.
Kati ya Septemba 2010 hadi 2011 alisoma na kuhitimu masomo ya uzamiri (MSc) ya Usimamizi wa Uwekezaji (Investment Management) katika Shule Kuu ya Biashara ya Cass (Cass Business School), London nchini Uingereza
Kabla ya hapo, Septemba 2007 – Juni 2010, Enock alisoma na kuhitimu Shahada ya kwanza (BSc) katika masuala ya Usimamizi wa Fedha (Finance and Management) katika Chuo Kikuu cha Cardiff, nchini Uingereza.
Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni tatu; Gemini Engineering s Construction ya Dar es Salaam) tangu 2017, Hoteli ya Kilimanjaro Wonders ya mjini Moshi tangu 2015 na Kampuni ya A1 Outdoor Tanzania ya Dar es Salaam tangu 2014, Enock anatajwa kuwa mjuzi na mahiri katika uongozi wa biashara, usimamizi wa miradi mikubwa na midogo, uandaaji wa bajeti, uchambuzi wa kifedha, na usanifu wa mikakati.
Kadhalika aliwahi kuwa Afisa Mwandamizi wa Sapien Capital Limited ya London, Uingereza (Aprili 2012 – Disemba 2013.
Jimbo la Vunjo
Jimbo la Vunjo ambalo lipo Wilaya ya Moshi, lina hitoria isiyo rafiki kwa wabunge wanaomaliza muda wao, kwani hakuna mbunge aliyewahi kupata uwakilishi wa vipindi viwili mfululizo tangu lilipoanzishwa mwaka 1995, hivyo Dkt. Kimei ana kibarua cha kuvunja mwiko huo.
Jimbo la Vunjo kabla ya kuanzishwa kwake, lilikuwa sehemu ya Jimbo la Moshi Vijijini ambalo kwa takriban miaka kumi (1985 – 1990 na 1990 – Machi 1995 lilikuwa chini ya uwakilishi wa Augustine Mrema.
Mrema hakumaliza kipindi chake cha pili kwani alijiuzulu ubunge wake Machi 1995 na kuhamia NCCR Mageuzi baada ya kutofautina na achama chake hadharani.
Katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Vyama vingi, jimbo hilo lilichukuliwa na James Mbatia kupitia NCCR Mageuzi, ambaye alifanikiwa tena kurejea katika nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kuwa mwakilishi mpaka 2020.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambao unatajwa kugubikwa na kasoro nyingi, Dkt. Kimei alichaguliwa kuwa Mbunge na anahitimisha uwakilishi wake Agosti 3, 2025.
Baada ya kufungua pazia la uwakilishi kupitia upinzani, katika Uchaguzi Mkuu wa 2000 Mbatia hakuweza kutetena nafasi yake na jimbo hilo, kwani lilitwaliwa na Meja Mstaafu, Jesse Makundi wa TLP (2000 -2005) ambaye pia alikaa kwa kipindi kimoja tu.
Katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, Meja mtaafu Makundi hakurejea kwani Vunjo walimchagua Aloyce Benti Kimaro (sasa ni marehemu) kupitia CCM kuwa mbunge wao kwa kipindi cha 2005 – 2010.
Kimaro baada ya kumaliza kipindi chake naye hakufanikiwa kurejea tena kwani Katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Augustino Mrema alichaguliwa kuwa Mbunge akiliwakilisha bungeni Jimbo la Vunjo kati ya 2010 – 2015. Mrema pia hakurejea kwani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Mbatia alirejea tena Vunjo.