Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi amewaataka wamekezaji kujitokeza katika kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi
Ameyasema hayo leo, June 29 wakati wakizindua kituo cha mafuta cha Kifaru Oil Investment Company LTD (Koil) kilichopo kata ya Kimochumi wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro chenye gharama milion 520.
Alisema kuwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan moja ya ahadi zake kwa wananchi ni kuwaruhusu wawekezaji wa ndani pamoja na wanje kuja kuwekeza nchini ambalo hapa tunamuona mwekezaji mzalendo ambaye ameamua kuiunga mkono Serikali
“Huyu mwekezaji wa kituo hiki cha mafuta ni mzalendo na mzawa wa moshi na ameonyesha upendo wake kwa serikali juu ya kuwekeza katika Taifa letu hivyo anastahili pongezi kubwa kwa hatua ya kuwekeza” alisema Ussi.
Alisema kuwa, wananchi wanahitaji huduma ya usafiri ambapo usafiri huo unahitaji mafuta na eneo hilo alilojenga kituo cha mafuta ni eneo la kimkakati katika uwekezaji wa mafuta.
Kiongozi huyo wa Mwenge alisema kuwa, uwekezaji huo unaleta faraja kubwa kwa Halmashauri ya Moshi kwani itaendelea kukua na kupitia uwekezaji kama huu itapelekea kupanda na kuwa Manispaa na hatimaye kuwa Jiji ambapo ndio matarajio ya Viongozi pamoja na Rais Dkt. Samia.
Ussi alitumia nafasi hiyo kuwaomba kama wapo wawekezaji wengine ambao wanajihisi wanaweza kuwekeza jambo lolote ndani ya Halmashauri ya Moshi wajitokeze kwani Dkt. Samia ameshatoa ruhusa.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji kwani wamewekeza fedha nyingi ambazo zinahitajika kuzalisha na kuipongeza kampuni ya Kifaru Oil Investment Company LTD (Koil) kwa kuuza mafuta safi.
Aidha alimtaka Mwekezaji huyo kutoishia kwenye sheli na kama wanahisi wanamradi mwingine ambao wanahitaji kuwekeza Ofisi ya Mkuu wa wilaya ipo wazi, na ya Mkurugenzi ipo wazi wataendelea kuwapokea.
“Kama mtahitaji maeneo ambayo mnahisi ni eneo la Serikali lakini mnaweza kuwekeza kwa jambo lolote nendeni kwa mkuu wa wilaya mwambieni naamini atawapeni maeneo hayo ili muweze kuwekeza” alisema Ussi.
Akisoma risala kwa niaba ya Mkurugenzi Suleman Mfinanga, Meneja wa Kampuni, Hassan Mfinanga alisema kituo hicho kilianza 2023 na ulikamilika kwa asilimia 100 kwa mwaka 2024 kwa ujazo wa lita 40,000.
Aidha aliishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwesha wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa utulivu