Tunduru – Ruvuma.
Jumla ya Wanachama 8 wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma, wamejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea Ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba Mwaka huu.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilayani Tunduru Yusuf Mabema amesema,kati ya wanachama hao 3 wanatoka Jimbo la Tunduru Kaskazini akiwemo aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo hilo Eng Ramo Makani na wanachama 5 wamechukua fomu kwa ajili ya kugombea Jimbo la Tunduru Kusini.
Mabema ametaja majina ya wanachama hao na majimbo wanayotaka kugombea ni Andulkadil Issa,Sikuzan Chikambo,Ramo Makan na Zamda Geuka kutoka Jimbo la Tunduru Kaskazini, Mohammed Njolo,Husna Kawanga,Bora Lichanda, Mtamila Abdul kutoka Jimbo la Tunduru Kusini.
Aidha alisema,hadi sasa wanachama 107 wamejitokeza kuchukua fomu za udiwani katika kata mbalimbali kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kupeperusha Bendera ya Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi huo.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu mmoja wa wanachamaMohammed Njolo alisema,ameamua kuomba kuchaguliwa kugombea Ubunge wa Jimbo la Tunduru Kusini ili awe mwakilishi mzuri wa wananchi.
Alisema,Jimbo la Tunduru Kusini kwa muda mrefu limebaki nyuma kimaendeleo kutokana na kukosa mtu sahihi wa kulisemea kwenye vikao vya maamuzi hasa kwenye Bungeni.
Alisema,iwapo chama kitamteua na kuchaguliwa na wananchi kwenye uchaguzi Mkuu ujao,atahakikisha analeta mabadiliko chanya kupitia uongozi kwa vitendo ikiwemo kutumia fedha za mfuko wa Jimbo kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Njolo alisema,Jimbo la Tunduru Kusini linahitaji kiongozi thabiti na mwenye uwezo na dhamira ya kweli atakayesimamia maslahi ya wananchi na kushughulikia changamoto zao kwa ufanisi.
Alisema,dhamira yake kubwa ni kutaka kuwatumikia wananchi na kushirikiana na kwa karibu na wanachama wa Chama cha Mapinduzi huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazofanya katika kuleta maendeleo.
Amewaomba wanachama na wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini,kuendelea kumuunga mkono katika hatua zinazofuata na kusisitiza dhamira yake ni kuwatumikia wananchi.
Kwa upande wake kiongozi wa kabila la Wayao Chifu Mtalika Mkwepu,amewaasa wananchi wa Jimbo hilo kutumia vizuri uchaguzi Mkuu kwa kuchagua viongozi bora watakaoleta maendeleo na kuwakataa wale wanaotaka kuchaguliwa kwa kutoa fedha na zawadi mbalimbali.
Alisema,wakati umefika kwa wananchi wa Jimbo hilo kuhakikisha wanampata kiongozi sahihi na mwenye uchungu kutokana na jimbo la Tunduru Kusini kukosa baadhi ya huduma muhimu za kijamii.