Na. Peter Haule na Chedaiwe Msuya, WF, Dar es Salaam
Wananchi wametakiwa kutumia taarifa zinazotolewa na Wizara ya Fedha kupitia njia mbalimbali za mawasiliano ili kupata taarifa mbalimbali za uchumi na fedha kwa lengo la kuawasidia kupata ufahamu na maarifa katika kukabiliana na changamoto za kiuchimi.
Hayo yamesemwa na Afisa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bi. Eva Varelian, alipokuwa akitoa elimu ya taarifa za uchumi, Sera, fedha na programu za Wizara, kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar Es salaam (Sabasaba) ambayo yameanza tarehe 28 Juni na kutarajiwa kuhitimishwa Julai 13 mwaka huu.
Alisema kuwa Wizara ya Fedha inazo taarifa nyingi kuhusu uchumi na fedha ambazo zinatolewa kwa wananchi kupitia nyenzo za mawasiliano za Wizara ambapo taarifa hizo zimekidhi vigezo kwa matumizi ya wananchi na taasisi za ndani na nje.
Alisema kuwa Wizara inatumia njia mbalimbali ambazo ni rahisi kwa watumiaji kulingana na mazingira yao, zikiwemo za Whatsap, Mtandao wa X (Tweeter), Linkidin, Hazina Tv, Instagram na Youtube.
Bi. Valerian alisema kuwa Wizara inatoa taarifa kwa njia ya Jarida la Hazina Yetu ambalo hutoka kila robo mwaka na pia inatumia Tovuti ambayo imesheheni taarifa mbalimbali zenye manufaa makubwa kwa wananchi wa hali zote.
Alisema kuwa taarifa za fedha na uchumi ni muhimu katika mipango ya maendeleo kwa wananchi wote wakiwemo wafanyabiashara, wanataaluma, watafiti, wakulima, wawekezaji na wajasiriamali.
Alieleza namna ya kuzifikia taarifa za Wizara kuwa ni pamoja na kutumia Tovuti ya Wizara ya Fedha (www.mof.go.tz) pamoja na akaunti za mitandao ya kijamii kama Facebook (MofURT), X (MofURT), Linkedin (Ministry of Finance Tanzania), Instagram (UrtMof) na Whatsapp Channel ( Wizara ya Fedha Tanzania).
Bi Valerian alisema kwa wale watakaobahatika kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya Sabasaba wanapata fursa ya kupata elimu ya njia za mawasiliano za Wizara kwa vitendo bila gharama zozote.
Aidha alisema kuwa Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya Sabasaba limesheheni wataalamu kutoka Idara na Vitengo vya Wizara hiyo na Taasisi zake ikiwa ni pamoja na Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Mfuko wa Dhamana na Uwekezaji Tanzania (UTT AMIS), Mfuko wa Self Microfinance, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX).
Taasisi nyingine ni pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Baraza la Masoko ya Mitaji (CMT), Benki ya Maendeleo TIB na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Hazina SACCOS, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).





(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)