NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Julai 2, 2025 kwenye Maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TET, Jamila Mbarouk amesema ushiriki wao katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada zake za kuendelea kuwasiliana moja kwa moja na wadau wa elimu, wakiwemo wazazi, walimu, wanafunzi, wachapishaji na wananchi kwa ujumla, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu majukumu yake pamoja na huduma mbalimbali inazotoa.
“Kupitia maonesho haya, wananchi wanapata fursa ya kujionea kazi za uchapishaji wa vitabu vya kiada na ziada, pamoja na mifumo ya kidijitali inayotumika kusimamia na kusambaza maudhui ya elimu nchini”. Amesema Jamila.
Aidha amesema wamekuwa wakitoa elimu kuhusu majukumu manne makuu ya TET yakiwemo uandaaji wa mitalaa, uandaaji wa vifaa vya saidizi vya kielimu,utoaji wa mafunzo kwa walimu nchini pamoja na kufanya Tafiti zinazosaidia kushauri Serikali katika suala la elimu.
Amesema kuwa TET imekuwa ikionesha mafanikio ya utekelezaji wa maboresho ya mitaala kwa shule za msingi na sekondari, ikiwa ni sehemu ya maboresho yanayolenga kutoa elimu bora, jumuishi na inayomuwezesha mwanafunzi kupata ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa.
Katika maonesho hayo, TET pia inatambulisha matumizi ya Tanzania Education Portal (TEP), jukwaa la kidijitali linalowawezesha walimu na wanafunzi kupata nyenzo mbalimbali za kujifunzia kwa njia ya mtandao, hatua inayokwenda sambamba na mapinduzi ya teknolojia katika sekta ya elimu.
Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la Taasisi ya Elimu Tanzania ili kujionea huduma mbalimbali na kupata elimu ya moja kwa moja kuhusu mustakabali wa elimu nchini.