Na Linda Akyoo-Kilimanjaro.
Miili 32 iliyochukuliwa vina saba katika hospitali ya Kanda ya KCMC kufuatia ajali ya basi la Kampuni ya Chanel One na Coaster kugongana na kuwaka moto Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro inakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu huku miili mingine miwili zoezi la kuchukua vinasaba linaendelea na miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu baadaa ya zoezi kukamilika.
Wanafamilia,marafiki na wananchi wanashiriki katika tukio hilo katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC kwa ajili ya kukabidhiwa miili ya ndugu zao .Majeneza yenye miili ya watu 36 kati ya 42 yamewekwa sehemu maalum ambapo wataagwa kimkoa na kisha kukabidhiwa familia kwa taratibu za maziko.
Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Katika mfululizo wa taarifa za ajali hiyo zilizokuwa zikitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu zilieleza kuwa waliofariki kwenye Coaster ni watu 31 ambao kati yao wanawake ni 21 na wanaume ni 10, huku kwenye basi la Chanel one wakifariki watu 11 na hivyo kufanya jumla ya waliofariki kufikia 42.