-Mkopo wa hadi Shilingi Milioni 133 kwa riba ya 5%-7% kutolewa
-Marejesho ni ndani ya miaka 7
-Lengo ni kuhakikisha bidhaa za mafuta zinapatikana kwa gharama nafuu
-Wananchi watakiwa kuchangamkia fursa
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mpango wa kuwezesha ujenzi na uendeshaji wa vituo vipya vidogo vya gharama nafuu vya bidhaa za mafuta (petrol na dizeli) maeneo ya vijijini ili kuondoa madhara yatokanayo na njia zisizo salama.
Hayo yamebainishwa Julai 3, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam ndani ya Banda la Maonesho la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Afisa Upimaji wa REA, Hussein Shamdas.
“Katika kuhakikisha nishati bora na salama inapatikana maeneo ya vijijini REA imeendelea kutekeleza majukumu yake ikihakikisha inaandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo mradi huu wa kuwezesha ujenzi na uendeshaji wa vituo vidogo vya bidhaa za mafuta maeneo ya vijijini,” alisema Shamdas.
Alitaja baadhi ya kadhia inayowakumbuka wakazi wa maeneo ya vijijini kufuatia kutokuwepo kwa vituo vya bidhaa za petrol na dizeli katika maeneo yao kuwa ni pamoja na gharama kubwa za upatikanaji wa bidhaa hizo tofauti na bei elekezi ya Serikali.
Mbali na suala la gharama, Shamdas alisema wakati mwingine bidhaa hizo zimekuwa zikiadimika maeneo ya vijijini kutokana na umbali uliopo kutoka kwenye vituo vya mafuta pamoja na gharama kubwa za usafiri.
“Kwa sasa uuzaji na uhifadhi wa bidhaa hizi za mafuta ya petroli na dizeli kwa vijijini sio safi na salama maana wengi wanahifadhi mapipa na madumu ya plastiki ndani ya nyumba jambo ambalo ni hatari linaweza kusababisha mlipuko na kugharimu maisha ya wananchi lakini pia sio salama kwa vyombo vya moto vinavyotumia bidhaa hizo,” alisema Shamdas
Madhara mengine ambayo Shamdas aliyataja ni pamoja na athari za kiafya kutokana na kuvuta hewa isiyo safi na salama kutokana na kuhifadhi bidhaa hizo ndani ya nyumba pamoja, athari za kimazingira zinazotokana na kumwagika kwa kwa mafuta maeneo mbalimbali pamoja na kuikosesha Serikali mapato kwa kuwa wauzaji wengi wa bidhaa hizo vijijini hawalipi kodi na tozo mbalimbali za Serikali.
“Kwa kutambua athari hizi na kwa kuzingatia malengo ya Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015, ni wajibu wa Wakala kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa nishati na kwa bei nafuu katika maeneo yote ya nchi kwa njia iliyo salama,” alibainisha.
Shamdas alitoa wito kwa wananchi kote Tanzania Bara kuchangamkia fursa ya kuomba mkopo huo ili kuweza kujenga na kuendesha vituo vya mafuta ambapo alisema mwananchi atapaswa kujaza fomu maalum na hatua zingine zitaendelea na kwamba mwongozo wa uombaji wa mkopo huo unapatikana kwenye tovuti ya wakaa ambayo ni www.rea.go.tz na pia kwa sasa mwananchi anaweza kutembelea banda la REA na kupatiwa mwongozo.