Katika kuimarisha uelewa wa matumizi ya bima kwa Jamii, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kushirikiana na Kampuni pamoja na watoa huduma za bima wamezindua rasmi Kijiji cha Bima katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 28 Juni 2024 kwa kuliambatana na shughuli mbalimbali za kihistoria na za kuvutia.
Tukio hilo lilihudhuriwa na watendaji wakuu (CEO’s) wa kampuni mbalimbali za bima chini ya Jumuiya ya Watoa Huduma za Bima Tanzania (ATI).
Uwepo wa wadau hao wa bima kwa katika tukio umeonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa watanzania zinaendelea kuwa za viwango, sikivu na zenye manufaa kwa wote.
Aidha, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Kanda ya Mashariki, Bw. Zakaria Muyengi ambaye alimuwakilisha Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware kuzindua rasmi Kijiji cha bima kwa kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi ameeleza kwamba TIRA imejipanga kuhakikisha elimu ya bima inawafikia watanzania wengi zaidi, kwa lengo la kuboresha ustawi na usalama wa kifedha na hali za wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi kutoka Sekta ya Bima nchini 2024, Bw. Agustino Ndabala, ambaye pia ni Afisa Biashara wa Kampuni ya Bima ya Grandree Insurance Tanzania, alieleza jinsi Kijiji cha Bima kilivyopangiliwa.
Kupitia maonesho haya, wananchi watapata fursa ya kukutana na wataalamu wa bima, kuuliza maswali, na kupata majibu yanayohusu bima kwa kina.