Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imeonya vikali wafanyabiashara wanaosafirisha mazao ya kilimo bila kusajiliwa, ikibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa COPRA, Irene Mlola, leo Julai 6, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Mamlaka hiyo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Mlola amesema kuwa COPRA inafanya juhudi kuhakikisha usalama wa chakula nchini na kwamba usafirishaji wa mazao bila usajili ni kinyume na sheria za nchi, zikiwemo Sheria ya Nafaka na Sheria ya Usalama wa Chakula.
“Unaposafirisha mazao bila kufuata taratibu, unajiingiza kwenye matatizo ya kisheria ambayo yanaweza kusababisha kufungwa kwa biashara yako, kutozwa faini au hata kufungwa gerezani,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa lengo la hatua hizo ni kuhakikisha kuwa biashara ya mazao nchini inafanyika kwa njia rasmi na yenye tija kwa uchumi wa taifa.
“Tunataka Tanzania ijulikane kimataifa kwa kuuza mazao yenye ubora yanayozingatia viwango vya kimataifa. Kwa sasa tumefungua milango ya masoko ya kimataifa kwa mazao kama vile ufuta, kokoa, choroko na mbaazi kupitia mfumo wetu wa kidijitali,” amesema.
Mlola amesema COPRA imefanikiwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na wale wa kimataifa ambao wamekuwa wakionesha nia ya kupata vibali vya usafirishaji wa mazao kutoka Tanzania.
“Tumeona watu wengi wakifika kutaka kujua namna wanavyoweza kushiriki biashara hii. Jibu letu ni moja: Jisajili kwanza,” amesisitiza.
Aidha ametoa wito kwa Watanzania wanaopenda kuingia katika biashara ya kusafirisha mazao kwenda nje ya nchi, kutembelea ofisi za COPRA zilizopo Makao Makuu, Dodoma na katika mikoa 14 nchini, au kupitia tovuti rasmi ya Mamlaka hiyo.
Ameeleza pia kuwa usajili huo unafanyika kupitia mfumo wa kidijitali wa E-Kilimo, ambapo wakulima na wafanyabiashara hujaza taarifa zao kwa ajili ya kupata kibali huduma ambayo ni bure.
“Milango iko wazi, tembeleeni banda letu hapa Sabasaba au ofisi zetu popote nchini ili mpate elimu ya kutosha kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya mazao,” amesema Bi. Mlola.
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanaendelea hadi Julai 13, 2025, yakihusisha wadau mbalimbali wa biashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) , Irene Mlola akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 6, 2025 wakati alipotembelea banda la COPRA, wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba Mbagala Jijini Dar es Salaam.