WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Wadau wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Afrika (ASSA), unaotarajiwa kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ridhiwani amesema kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kufungua rasmi mkutano huo Julai 10, 2025
Amesema mifuko ya hifadhi ya jamii itakayoshiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni pamoja na NSSF, PSSF, NHIF, WCF, ZSSF, na ZHHF.
Aidha, mkutano huo utahusisha ushiriki wa wadau wa sekta hiyo, ambao pia watahudhuria kongamano litakalofanyika Julai 9 mwaka huu jijini humo, ambapo pamoja na mambo mengine mada mbalimbali zinazohusiana na mifuko ya hifadhi ya jamii zitajadiliwa kwa kina.
Ridhiwani amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau, watunga sera, wasimamizi na watendaji wa sekta ya hifadhi ya jamii Afrika, ili kwa pamoja wajadili na kuazimia namna sekta hiyo ilivyokuwa na uwezo mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma nyingine za kijamii katika Bara la Afrika.
Jumuiya ya ASSA inaundwa na mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi 15 za Bara la Afrika ambazo ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Sudan ya Kusini, Comoro, Sierra Leone, Côte d’Ivoire, Gambia, Mali, Namibia, na wenyeji wao wa mkutano huo kutoka Tanzania.