· Waziri wa Mambo ya nje wa Cyprus, Dkt. Constantinos Kombos anatarajiwa kuanza ziara yake Rasmi nchini Tanzania kuanzia tarehe 8 hadi 10 Julai, 2025 kwa niaba ya Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya wa Mambo ya Nje na Usalama / Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya, Kaja Kallas
· Katika ziara hiyo Waziri Dkt. Constantinos Kombos atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na viongozi wengine wa serikali, mazungumzo yao yataangazia uhusiano wa EU na Tanzania, utawala bora wa kidemokrasia, na ushirikiano wa kiuchumi chini ya mkakati wa Global Gateway.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus, Dkt. Constantinos Kombos, atatembelea Tanzania kuanzia tarehe 8 hadi 10 Julai kwa niaba ya Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU) wa Mambo ya Nje na Usalama / Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya, Kaja Kallas, katika jitihada za kuimarisha ushirikiano kati ya EU na Tanzania na kushiriki katika mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa.
Wakati wa ziara hiyo, Waziri Dkt. Constantinos Kombos atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia, viongozi wa biashara na wadau wengine kujadili uhusiano wa EU na Tanzania, uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ushirikiano wa kiuchumi chini ya mkakati wa Global Gateway, na maendeleo ya usalama katika eneo la Maziwa Makuu.
Akizungumza kabla ya ziara, Waziri Dkt. Constantinos Kombos alisema:
“Tanzania ni mshirika wa kuaminika na thabiti katika eneo lenye umuhimu mkubwa. Tunaposherehekea miaka 50 ya uhusiano kati ya EU na Tanzania mwaka huu, EU imejizatiti kuimarisha ushirikiano wetu – kuanzia uwekezaji katika malighafi muhimu na mabadiliko ya kidijitali hadi kuendeleza maadili ya kidemokrasia na ukuaji wa pamoja. Pamoja tunaweza kufungua fursa mpya zitakazowanufaisha wananchi wa Tanzania na washirika wa Ulaya.”
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau, alisisitiza umuhimu wa ziara hiyo:
“Ziara hii inaakisi dhamira ya EU ya ushirikiano imara na wa kimkakati na Tanzania, unaojengwa kwa maslahi ya pande zote. Kufuatia ziara ya Waziri Kombo katika Makao Makuu ya EU mwezi Aprili, hii ni ishara ya kuendelea kwa mazungumzo endelevu kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania.”
Katika ziara hii, masuala ya siasa yanayohusiana na pande zote, maendeleo ya kikanda, na ushirikiano wa kiuchumi yatajadiliwa.
Hii ziara inafuatia mikutano ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, iliyofanyika Brussels mwezi Aprili 2025 na Mwakilishi Mkuu wa EU wa Mambo ya Nje na Usalama Kaja Kallas, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa Koen Doens, na Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya )EIB) Thomas Östros, lengo la Mkutano huu ilikuwa ni kuendeleza mazungumzo ya kisiasa, uwekezaji, na maendeleo endelevu.