Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) Brigedia Jenerali George Itang’are akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya Maafisa wanadhimu jijini Dar es Salaam leo Julai 01, 2025.
Upande wa Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo Jumuishi kutoka Umoja wa Mataifa (“Chief Integrated Training Services, UN), Harinder Sood akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya Maafisa wanadhimu jijini Dar es Salaam leo Julai 01, 2025.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
CHUO cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC), kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, kimezindua rasmi mafunzo ya Ukufunzi kwa Maafisa Wanadhimu wa Umoja wa Mataifa. Mafunzo hayo yatafanyika kuanzia leo Julai 7 hadi 17, 2025 katika chuo hicho kilichopo jijini Dar es Salaam.
Akifungua rasmi mafunzo hayol eo Julai 7, 2025 Mkuu wa Chuo cha TPTC, Brigedia Jenerali George Itang’are, amesema kuwa hii ni mara ya pili kwa kozi hiyo kuendeshwa duniani tangu Umoja wa Mataifa ulipoandaa mtaala mpya, ambapo kozi ya kwanza ilifanyika nchini Italia.
“Kozi hii ni ya kwanza kufanyika hapa Tanzania tangu ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa. Ni kozi muhimu sana kwa sababu washiriki wake wanatoka katika mataifa mbalimbali,” amesema Brigedia Jenerali Itang’are.
Washiriki wa mafunzo haya wanatoka katika nchi za Ghana, Nigeria, Vietnam, Botswana, Zambia na Tanzania.
Lengo kuu la kozi hiyo ni kuwajengea uwezo wakufunzi wa maafisa wanadhimu wa Umoja wa Mataifa, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.
“Kozi hii inalenga kuwapa maarifa ya ukufunzi maafisa wenye uzoefu, ambao wanatarajiwa kuendesha mafunzo ya wanadhimu katika nchi zao, ikiwemo hapa Tanzania,” ameongeza Itang’are.
Ameeleza kuwa katika mfumo wowote wa kijeshi au amani, kuna kamanda na wanadhimu, hivyo kozi hii inawalenga wale wanaotarajiwa kufanya kazi katika sekta hiyo pamoja na makao makuu ya vituo vya amani duniani kote.
Itang’are pia amebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofaidika na mafunzo haya. Aidha, wakufunzi kutoka Tanzania nao wameshiriki kikamilifu, hivyo kuwezesha nchi kuwa na uwezo wa kuendesha mafunzo ya kisasa kwa viwango vinavyotakiwa kimataifa.
Jumla ya wanadhimu 22 wanashiriki katika kozi hiyo, wakiwemo wakufunzi wa kimataifa saba na wakufunzi wawili kutoka Tanzania.
Kwa Upande wa Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo Jumuishi kutoka Umoja wa Mataifa (“Chief Integrated Training Services, UN), Harinder Sood ameeleza kuwa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa wa sasa unakabiliwa na changamoto nyingi tofauti na enzi za zamani, ambapo operesheni hizo zilikuwa za jadi na zenye mazingira mepesi zaidi.
Amesema kuwa Maafisa wanadhimu waliobobea, wenye uwezo na weledi ni jambo muhimu sana kwa mafanikio ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.
“Nimefurahishwa sana kuona kuwa mafunzo ya kwanza ya aina hii yanayoendeshwa na idara yangu hapa Tanzania. Wakufunzi hawa watakaporejea katika nchi zao, watatoa mafunzo kwa maafisa wengine ambao watakuwa tayari kwa ajili ya kutumwa katika operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa kama maafisa wanadhimu,” amesema Sood
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia nchi wanachama kuendesha kozi hizo kitaifa, lakini pia kushiriki katika mafunzo ya kimataifa, hivyo kuongeza uwezo wa pamoja wa kupeleka maafisa waliobobea kwenye operesheni za kulinda amani duniani kote.
Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania imekuwa na historia ndefu na ya mafanikio katika kushiriki kwenye operesheni za ulinzi wa amani.
Amesema kuwa Tanzania ni nchi imara na salama, jambo ambalo limeifanya kuwa kitovu kizuri kwa mafunzo ya kimataifa, sio tu kwa nchi jirani bali pia kwa washiriki waliotoka mbali kama Vietnam.
Matukio mbalimbali katika picha.
.jpeg)
Burudani ikiendelea.