Pamela Mollel,Arusha.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ismail Ally Ussi, amezitaka sekta binafsi nchini kutumia vema fursa ya uboreshaji wa sera na mazingira ya uwekezaji nchini .
Amesema kuwa serikali ya awamu hii imefanya kazi kubwa ya kuondoa vikwazo vingi vya uwekezaji ili kuvutia wadau wengi kufanya kazi na biashara nchini.
Ussi ameyasema hayo baada ya kuzindua kituo cha kisasa cha mafuta cha Petro Africa (T) Ltd kilichojengwa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi 800 milioni wilayani Longido, mkoani Arusha walipotembelea na msafara wa mwenge wa Uhuru.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa kituo hicho kilichojengwa katika Kata ya Kimokouwa, Ussi amesema kuwa kuwa mradi huo ni ushahidi wa namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki kikamilifu katika jitihada za kitaifa za maendeleo.
“Nawapongeza kwa uwekezaji huu wa mfano kwani mmeonesha uzalendo wa hali ya juu na mmejitokeza kuwa sehemu ya historia ya Mwenge wa Uhuru kwa vitendo”amesema na kuongeza;
“Hii ni njia mojawapo ya kumuunga mkono Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hivyo niwaombe na wengine wahakikishe wanatumia fursa hii vuzuri” amesema Ussi.
Mbali na hilo, Ussi amewataka wananchi wa wilaya ya Longido kuwaunga mkono wawekezaji wanaojitokeza kutatua kero mbalimbali katika jamii zao ikiwemo kununua bidhaa wanazoleta.
“Hapa amejitokeza muwekezaji huyu kajenga kituo hiki ambacho kitaondoa kero ya upatikanaji wa mafuta, niwaombe mje kununua mafuta hapa, maana hadi kuita mwenge wa uhuru kuzindua maana yake mafuta yake yako safi na yana viwango vya hali ya juu” amesema.
Akisoma taaarifa ya mradi huo mbele ya wakimbiza mwenge kitaifa na viongozi wa serikali, Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa PetroAfrica (T) Ltd, Abdi Hassan Ibrahim, amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Machi 2024 na kukamilika mwezi Juni 2025, kwa gharama ya shilingi milioni 800.
Amesema ujenzi huo umehusisha visima vya kuhifadhia mafuta, pampu za kisasa, maeneo ya maegesho, ofisi za kisasa, pamoja na miundombinu ya usalama.
“Lengo ni kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za nishati ya mafuta kwa wananchi na sekta ya usafirishaji, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya”.
“Tunashukuru Serikali ya awamu ya sita kwa mazingira bora ya uwekezaji yaliyopelekea kufanikisha mradi huu. Mbali na kuongeza huduma ya nishati, tumetoa ajira kwa wananchi wa Longido na kusaidia taasisi za umma na sekta binafsi kupunguza changamoto za upatikanaji wa mafuta,” amesema Ibrahim.