*Mfanyabiashara wa madini anaswa mkoani Lindi akisambaza biskuti hizo
Na Emmanuel Mbatilo, Dar es Salaam
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)imebaini uwepo wa kiwanda bubu kinachotengeneza biskuti zinazochanganywa na bangi kisha kuzisambaza katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara.

Akizungunza leo Julai 9,2015 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo Aretas Lyimo kiwanda hicho wamekibaini eneo la Sinza na tayari watu wawili ambao ni wamiliki wa kiwanda hicho wanashikiliwa na sheria itachukua mkondo wake.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema katika operesheni waliyoifanya Julai 8 mwaka huu walibaini kiwanda hicho ambako wakati wamefika kiwandani walikuta shughuli za kutengeneza biskuti hizo ukiendelea hivyo walisimamisha uzalishaji huo na kukiweka chini ya ulinzi.
“Katika operesheni ambayo tumeifanya katika eneo la Sinza Dar es Salaam tumekikuta kiwanda bubu cha kutengeneza biskuti ambazo zimechanganywa na bangi na biskuti hizo huzissmbaza kwa wananchi ili kutengeneza uraibu.
“Hata hivyo mkoani Lindi tumemkamata mfanyabiashara wa madini akisambaza biskuti zilizochanganywa na bangi.Hivyo naye tunamshikilia na huenda pia wanatumia biskuti hizo kuwapa watu ambao wanafanya nao biashara ya madini ili kuwalewesha na hatimaye kuwaibia.”
Awali wakati akieleza operesheni zinazofanywa na Mamlaka hiyo Kamishna Jenerali Lyimo amesema katika kipindi cha Mei hadi Julai, 2025, Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini na kukamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu 37,197.142.
Amesema dawa hizo zinajumuisha, kilogramu 11,031.42 za dawa mpya za kulevya (New Psychoactive Substance) aina ya Mitragyna Speciosa, bangi kilogramu 24,873.56, mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, heroin kilogramu 2.21 na methamphetamine gramu 1.42.