JESHI la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo kwamba wamemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, wakitaka ufafanuzi juu ya madai kuwa viongozi wao wametakiwa kuwasilisha taarifa na majina ya watia nia ya kugombea ubunge na udiwani kwa Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi linapenda kufafanua kuwa hadi sasa, barua hiyo haijamfikia rasmi Mkuu wa Jeshi la Polisi. Endapo barua hiyo itapokelewa, maudhui yake yatafanyiwa kazi kwa haraka kwa lengo la kupata ukweli wake, ikiwemo kubaini chanzo cha mawasiliano hayo na nani aliyeyatoa.
Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza kuwa linafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo, na litaendelea kushirikiana na vyama vyote vya siasa kwa misingi ya haki, usawa na kuheshimu misingi ya kidemokrasia.