-Ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini
Dar es Salaam, Julai 10, 2025
Tume ya Madini imejipanga kwa dhati kuhakikisha Watanzania wanapewa kipaumbele katika usambazaji wa bidhaa na huduma katika migodi ya madini ili kuwajengea uwezo wa kiuchumi, kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi na kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kupitia Sekta ya Madini.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, Meneja wa Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa Tume hiyo, Bw. Greyson Mwase amesema Serikali kupitia Tume ya Madini inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria ya Madini, Sura ya 123 Kifungu cha 102 pamoja na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018.
“Lengo kuu la kanuni hizi ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa madini kupitia utoaji wa bidhaa na huduma migodini badala ya kuziacha kampuni kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,” amefafanua Mwase.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume ya Madini, katika mwaka wa fedha 2023/2024, migodi ya madini nchini ilizalisha ajira rasmi 19,874 ambapo kati ya hizo, ajira 19,371 sawa na asilimia 97 zilitolewa kwa Watanzania, huku wageni wakipewa ajira 503 tu sawa na asilimia 3.
Bw. Mwase ameongeza kuwa kampuni za madini nchini hutumia wastani wa shilingi trilioni 5.3 kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazotumika migodini, na hivyo kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo kwa kuanzisha au kuimarisha biashara zinazohusiana na sekta hiyo.
Aidha, ameshauri taasisi za kifedha nchini kuongeza wigo wa utoaji mikopo na mitaji kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya madini, hasa katika maeneo ya usambazaji wa vifaa, huduma za vyakula, usafiri, usafi na nyinginezo zinazohitajika katika migodi.
Tume ya Madini inaendelea kuelimisha umma kuhusu fursa hizi kupitia maonesho mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maonesho ya Sabasaba, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wananufaika na rasilimali za taifa lao.