-Miaka minne ya Rais Samia utalii tiba waendelea kupaa
Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Utalii Tiba Kitaifa imekabidhi ripoti ya miaka minne kwa serikali ikielezea mafanikio lukuki ikiwemo ya tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba kusini mwa jaangwa la sahara.
Ripoti hiyo ilikabidhiwa jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdulmalik Mollel kwa Waziri wa Afya, Jenister Mhagama mjini Dodoma.
Mollel alisema Kamati ya Tiba Utalii Tiba iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Profesa Mohamed Janabi ilianza 2021 imemaliza muda wake mwaka 2024.
Alisema kamati hiyo iliyoanzishwa na Wizara ya afya ilikuwa na jukumu la kuangalia namna Tanzania inavyoweza kuangalia fursa za utalii tiba
Molle alisema Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Mei mwaka 2021 na kuzindua mtambo na ndipo alisema kuwa anatamani kuona Tanzania inakuwa kituo cha tiba utalii hasa kusini mwa jangwa la sahara
“Baada ya kuona uwekezaji mkubwa uliofanyika JKCI ndipo alipotoa maono hayo kwa hiyo kamati hii ambayo imemaliza muda wake ilundwa kutokana na maono ya Rais Samia,” alisema Mollel
Aidha, Mollel alisema miongoni mwa majukumu ya Kamati hiyo yalikuwa ni kuangalia uwezo na mapungufu ya Tanzania katika kutekeleza utalii tiba.
Alisema ili kutekeleza maono hayo, kwa kuanzia walipendekeza hospitali nne ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa (MOI).
Alisema Kamati hiyo ilitembelea nchi mbalimbali kujifunza kuhusu utalii tiba kwenye nchi zilizoendelea na zilizopiga hatuaa kubwa kwenye sekta ya afya ikiwemo India ambako walikwenda na madaktari bingwa bobezi 18.
Alisema kamati hiyo ilipewa kazi ya kupendekeza sera na mifumo ya kisera na kitaasisi kama inafaa kwa utekelezaji wa utalii tiba na kama kunahitajika maboresho.
“Tulipewa jukumu la kushauri kuhusu hatua za wali za masoko na uratibu wa wadau na ujenzi wa uwezo ili tukisema tuko tayari twende kwenye utekelezaji moja kwa moja,” aliema Mollel
Alisema kwenye hospitali za majaribio zilizoteuliwa zilitumika kama vituo vya majaribio na kila hospitali iliratibu maandalizi ya utalii tiba na kuongeza kuwa walitamani kuingiza hospitali binafsi ila waligundua kuwa hospitali hizo mbili tayari zinafanya utalii tiba.
Alisema Kamati iliratibu maboresho ya ndani ya miundombinu katika hospitali hizo kama vyumba vya VIP na walifanya mikutano na wadau na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi na mabalozi wa nje ya nchi walioko nchini Tanzania.
“Tuliandaa rasimu ya mfumo wa utekelezaji wa kitaifa ila bado nyaraka hizo ziko kwenye rasimu na tulibaini kuwa serikali ya awamu ya sita imewekeza vya kutosha kwenye sekta ya afya na inakidhi kuanza kuifanya kuwa kituo cha tiba utalii kusini mwa jangwa la sahara,” alisema.
Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema Kamati ya Utalii Tiba iliendesha program ya Dk Samia Outreach Programu nchini Comoro kwaajili ya kutangaza uwekezaji ambao umefanywa nchini
Alisema akiwa nchini Comoro madaktari wa Tanzania waliwaona watu 2,770 ambao kati yao 470 walihitaji rufaa ya kwenda kwenye hospitali za JKCI, Benjamin Mkapa, MKOI, Muhimbili na Ocean Road.Dk Kisenge alisema nchini Comoro walitumia gharama ya shilingi milioni 300 lakini mpaka sasa pesa zilizokusanywa kutokana na utalii tiba zinafikia zaidi ya shilingi bilioni mbili.
“Maana yake hizi hela zilizopatikana zinarudi kusaidia kuwapa matibabu watu wasiokuwa na uwezo wa kupata matibabu, nawashukuru sana viongozi wa hospitali zote tuliofanya nao kazi, wenzetu wa sekta binafsi Global Medicare ilifanya branding ya kazi ya utalii tiba na kwa sasa mataifa mbalimbali yanataka kuja kutibiwa hapa,” alisema
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alisema ili kufikia ndoto kamili za utalii tiba lazima kuwekeza kwenye ukarimu wa wageni kama ambavyo mashirika yanayofanyaa vizuri hasa yaa ndege yamekuwa yakifanya.
“Kwenye ndege ukiingia unakuta wahudumu muda wote wanatabaasamu mpaka unajiuliza wameumbwaje hawa, mgonjwa anapokuja pale mapokezi ni sehemu ya yeye kupunguza msongo wa mawazo . Mtu mwenye msongo wa mawazo akikutana na mtu mkarimu anaanza kupata nafuu kutoka hapohapo,” alisema
Alisema asilimia 80 ya watanzania wanaweza kupata huduma za afya chini ya umbali wa kilomita tano kutoka wanapoishi na kwamba Tanzania si miongoni mwa nchi za Afrika ambazo hazina mashine za MRI.
Waziri Mhagama alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa JKCI Dk Peter Kisenge kwa kutoa matibabu ya kibingwa kiasi cha kuwavutia wagonjwa wa kimataifa kwenda kutibiwa JKCI.
“Nilimtaja Abdulmalik Mollel mwanzoni ila niendelee kukutaja tena na tena na tena na nitatoa maagizo ya uundaji wa kamati. Katibu Mkuu kwa kuwa tutahitaji sekta binafsi itusaidie kama itawapendeza kitaalamu nitakapomtaja Mwenyekiti aongoze Kamati hii sasa naamini Mollel bado anafaa kutusaida, kutushauri na kutuongoza kutupeleka tunakotaka kwenda nahii simpigii debe nazungumzia uhalisia. Mollel nakushukuru sana sana kwa kazi nzuri sana,” alisema