WASANII mahiri wa muziki wa Bongo Fleva, Chege Chigunda na Madee, wanaofahamika kwa jina la kisanii Samia Kings, wamevutia umati wa mashabiki na washiriki wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa ujumbe mahiri wa kuhamasisha Watanzania kuenzi na kutumia bidhaa zenye nembo ya Made in Tanzania.
Wasanii hao walitembelea banda la Made.In Tanzania linaloongozwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na kupokelewa rasmi na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana. Banda hilo limejikita kuonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na Watanzania kwa ubunifu wa hali ya juu na viwango vya kimataifa.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Madee aliwasihi Watanzania kutembelea maonesho hayo na kushuhudia bidhaa za asili ya Kitanzania.
“Kama bado uko nyumbani na hujafika kwenye banda letu la Made in Tanzania, umepata dhambi! Kuna vitu vingi sana vya asili yetu ambavyo huwezi kuviona popote. Hii ni fursa ya kipekee kujifunza na kujivunia vyetu,” alisema.
Madee alisimulia pia uzoefu wake nje ya nchi ambapo alinunua bidhaa alizojua zinatoka Tanzania lakini zikiwa zimebeba nembo ya mataifa mengine:
“Nilinunua nyanya na vitunguu ambavyo nilijua kabisa vimetoka Tanzania, lakini zikaandikwa Made in nchi nyingine. Hii inaumiza. Ndiyo maana huu mpango wa Made in Tanzania ni ukombozi mkubwa kwa sisi waishio nje na wenye mapenzi na bidhaa za nyumbani.”
Kwa upande wake, Chege alielezea namna Sabasaba ni tukio la kipekee kwake kwani linafanyika “nyumbani kwake, Temeke”. Alisema kuwa alitamani kwenda na binti yake Jada ili kumjengea utamaduni wa kupenda vya kwao.
“Ningekuja naye tungenunua bidhaa nyingi za Kitanzania. Watoto wana adopt mapema, hivyo huu ni wakati mzuri wa kuwajengea moyo wa kupenda vya kwao. Nawaomba wazazi wenzangu tuwalete watoto wetu, ndiyo kizazi cha kesho.”
Chege pia alionesha kuvutiwa sana na ubunifu wa mavazi, viatu, na bidhaa nyingine kutoka kwa wabunifu na wazalishaji wa ndani.
Katika hatua ya kuvutia, msanii mmoja kutoka Afrika Kusini aliyeshiriki katika maonesho hayo, alieleza kuvutiwa sana na ubora wa bidhaa za Tanzania na kuahidi kuwa balozi wa kuzitangaza nchini kwake.
“Nimeona vitu vya hali ya juu, na nimepata uzoefu mzuri. Nitarudi na kuwaeleza watu wetu Afrika Kusini kuwa Tanzania inatengeneza bidhaa bora kabisa,” alisema.
Naye Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Mapana, alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kutembelea banda hilo la Made In Tanzania ( Karume)
“Maonesho yanaendelea hadi Julai 13. Muda bado upo, na tunawakaribisha Watanzania wote kutembelea na kujivunia Made in Tanzania.”
Banda hilo limekuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya mwaka huu, likiwakutanisha wabunifu, wajasiriamali na wanamuziki kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya bidhaa za ndani na kuchochea uchumi wa viwanda unaojengwa na Watanzania wenyewe.