Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wameandaa jukwaa maalum la mafunzo ya siku tatu kwa wataalamu wa masuala ya fedha, kodi na ukaguzi wa hesabu, likiwa na lengo la kujadili bajeti ya 2025/2026 na kutoa mapendekezo kwa ajili ya bajeti ya 2026/2027, hali ya uchumi na masuala ya kodi.
Mafunzo hayo, yanayofanyika kuanzia leo Julai 16 hadi 18, 2025, yanahusisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali kwa ajili ya kujadili masuala ya bajeti, uchumi, kodi na changamoto za kisheria zinazoathiri ukusanyaji wa mapato.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa hilo, Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka TRA, Bw. Alfred Mregi aliyemwakilisha Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema kuwa ushirikiano kati ya Mamlaka na Bodi hiyo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa. Alieleza kuwa kupitia mijadala hiyo, wataalamu wanapata nafasi ya kuibua mikakati ya kitaalamu itakayoboresha utendaji katika sekta ya kodi na fedha kwa ujumla.
“Mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yanahitaji ushirikiano wa karibu na taasisi kama NBAA. Majukwaa haya yatatusaidia kupata suluhisho la changamoto zinazokwamisha ufanisi katika mifumo ya kodi,” alisema Bw. Mregi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na majukwaa mahsusi ya wadau wa sekta ya kodi kwa ajili ya kujadili changamoto zinazojitokeza na kutoa mapendekezo ya maboresho kwa mamlaka husika.
“Lengo letu ni kuwa na majadiliano ya moja kwa moja ambapo changamoto zitajibiwa papo kwa papo, na yale yanayohitaji hatua zaidi kuwasilishwa kwa mamlaka za juu kama TRA. Hii ni njia ya kuongeza mapato kwa haraka, bila kuongeza mzigo kwa walipakodi,” alisisitiza CPA Maneno.
Aliongeza kuwa NBAA, kama Bodi ya kitaaluma, imekuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha. Kupitia jukwaa hili, NBAA inakusanya maoni kutoka kwa wahasibu, wakaguzi wa hesabu na wadau wa sekta binafsi, kwa lengo la kuyawasilisha serikalini ili kufanikisha maboresho ya sheria na sera za kodi.
Kupitia ushirikiano huu, taasisi hizo mbili zinatarajia kufanikisha mabadiliko chanya yatakayoliwezesha taifa kukusanya mapato zaidi kwa njia rahisi, ya haki, na yenye tija kwa maendeleo ya kiuchumi.
Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka TRA, Bw. Alfred Mregi akizungumza na wahasibu, wakaguzi na washauri wa kodi alipokuwa anafungua jukwaa maalumu la mafunzo ya siku tatu lenye lengo la kujadili masuala ya bajeti, uchumi na Kodi lililoandaliwa na NBAA kwa kushirikiana na TRA na kufanyika katika ukumbi wa APC Bunju jijini Dar ea Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno akizungumza na wahasibu, wakaguzi na washauri wa kodi pamoja na kumkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya kufungua jukwaa maalumu la mafunzo ya siku tatu lenye lengo la kujadili masuala ya bajeti, uchumi na Kodi lililoandaliwa na NBAA kwa kushirikiana na TRA na kufanyika katika ukumbi wa APC Bunju
Baadhi ya wahasibu wakaguzi na washauri wa kodi wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi alipokuwa anafungua jukwaa maalumu la mafunzo ya siku tatu lenye lengo la kujadili masuala ya bajeti, uchumi na Kodi lililoandaliwa na NBAA) kwa kushirikiana na TRA.
Mgeni Rasmi Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka TRA, Bw. Alfred Mregi (katikati waliokaa) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (wa pili kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja wahasibu, wakaguzi na washauri wa kodi waliofika kwenye jukwaa maalumu la mafunzo ya siku tatu lenye lengo la kujadili masuala ya bajeti, uchumi na kodi yaliyoandaliwa na NBAA kwa kushirikiana na TRA na kufanyika katika ukumbi wa APC Bunju leo Dar es Salaam.