-Serikali kupunguza ada ya kodi ya pango kwa mwaka kwa Leseni ya chumvi
-Rais Samia apongezwa kwa kiwanda cha kusafisha chumvi Lindi
-Wazalishaji wa chumvi wafurahia kuanza kwa kodi ya zuio
-Serikali kudhibiti uingizaji wa chumvi kiholela nchini
Dar es Salaam
Katika kuwajengea uwezo wazalishaji wa chimvi nchini,Serikali imekuja na mikakati mbalimbali kufikia azma hiyo ikiwemo upunguzaji wa ada ya pango kwa mwaka ya leseni (Annual Rent) za uchimbaji mdogo wa chumvi nchini ili kusaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji wa wingi wa chumvi nchini.
Hayo yamesemwa jana tarehe 15 Julai, 2025 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde (Mb) Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga Kikao cha wadau wa sekta ndogo ya chumvi chini ya Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA).
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutubeba sekta ya madini na wachimbaji kwa ujumla. Ni yeye aliyetuelekeza kusikiliza kilio chenu na kutatua changamoto zinazowakabili ili mnufaike na shughuli mnazofanya”
“Ametuelekeza Wizara ya Madini tuliridhie ombi lenu na kupunguza ada ya pango ya mwaka ya leseni ya uchimbaji mdogo kutoka Shilingi 45,000 mpaka Shilingi 20,000 kwa hekta, hili linakwenda kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ubora wa chumvi ya mzalishaji mdogo” alieleza Mhe. Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo udhibiti wa chumvi inayoingizwa kutoka nje ya nchi, zimepelekea bei ya chumvi ghafi kuongezeka na hivyo kuwanufaisha zaidi wazalishaji wadogo wa chumvi nchini.
Uanzishwaji wa kodi ya zuio ya asilimia mbili (2%) kwenye mauzo ya chumvi ghafi kwa wazalishaji wenye leseni za PML imekuwa ni neema na manufaa kwao badala ya utaratibu wa awali wa kufanyiwa makadirio ya kodi ya mapato, ambao ulikuwa ni kero kubwa kwa wazalishaji wadogo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde alieleza kuwa Kiwanda cha kuzalisha chumvi cha STAMICO kipo hatua za mwisho, na kuagiza Shirika hilo kuhakikisha kabla ya mwezi wa Agosti kuisha kiwe kimekamilika na kuanza uzalishaji wa chumvi ili kupanua wigo wa soko la chumvi ya wazalishaji wadogo.
Awali, akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi yao, Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA), Bi. Hawa Ghasia aliishukuru Serikali kwa kushughulikia changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta ndogo ya chumvi nchini ambazo zimepelekea bei ya chumvi kupanda na kuwanufaisha zaidi wazalisha chumvi nchini.