Na Diana Byera – Bukoba
Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, limekabidhi vifaa vya afya vyenye thamani ya shilingi milioni 112 kwa halmashauri za Biharamulo na Muleba, mkoani Kagera. Vifaa hivyo vitatumika katika kufanya uchunguzi wa afya kwa wagonjwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha hali ya kawaida baada ya mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg.
Mwakilishi mkazi wa WHO nchini, Dkt. Galberth Fadjo, alisema kuwa shirika hilo limekuwa bega kwa bega na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, katika kuhakikisha magonjwa hatari kama Marburg yanadhibitiwa mapema ili yasisambae zaidi. Pia alisisitiza kuwa WHO itaendelea kutoa msaada wa haraka wakati wa dharura, hasa katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Akitoa mfano wa milipuko iliyotokea Kagera – Bukoba mwaka 2023 na Biharamulo mwaka 2024 Dkt. Fadjo alisifu namna serikali ilivyoweza kupambana na ugonjwa huo bila kuathiri shughuli nyingine za kijamii, na hatimaye kurejesha hali ya kawaida, alisema mfano huo ni wa kuigwa na nchi nyingine zinazokabiliana na majanga ya kiafya.
Aidha, aliwataka wataalamu wa afya kutumia vifaa hivyo kwa weledi na kutoa elimu kwa watakaovitumia, sambamba na kuendelea kuweka mazingira salama katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, alieleza kuwa vifaa vilivyopokelewa ni pamoja na Vitanda vya kisasa vya kulaza wagonjwa,
Mashine za kusafisha mashuka, Stendi za kuwekea dawa, ndoo za kuhifadhi maji na kufanyia usafi, vifaa vya kufanya uchunguzi wa kina.
Alisema vifaa hivyo ni sehemu ya mkakati wa kurejesha hali baada ya mlipuko, na vimetolewa sambamba na mafunzo mbalimbali ambayo Wizara ya Afya imekuwa ikiyatoa kwa wananchi kuhusu kutoa taarifa mapema pale wanapoona dalili za ugonjwa usio wa kawaida. Aidha, alieleza kuwa wizara imeongeza juhudi katika kuimarisha utayari wa kitaifa, kushirikisha jamii, na kuunganisha wadau wote katika kudhibiti milipuko ya magonjwa.
Alibainisha kuwa vifaa hivyo vitaongeza ufanisi wa kazi kwa wataalamu wa afya mkoani Kagera, huku akilishukuru shirika la WHO kwa usaidizi wake mkubwa katika kipindi chote cha mlipuko wa ugonjwa huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Steven Ndaki, alitoa wito kwa wataalamu wa afya kuvitunza na kutumia vifaa hivyo kwa ufanisi, huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa ya mlipuko – hata kama kwa kipindi hicho hakuna ugonjwa ulioripotiwa.
Ndaki alisema mkoa wa Kagera utaendelea kujiweka tayari kukabiliana na dharura za milipuko, hasa kutokana na jiografia yake ya kupakana na nchi nyingi, hali inayoongeza hatari ya kusambaa kwa magonjwa ya milipuko.