Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja amesema,wilaya hiyo inakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia kilimo cha zao la korosho, baada ya Serikali kutoa pikipiki kwa maafisa ugani ili waweze kuwafikia wakulima kwa urahisi.
Masanja,amesema hayo wakati akikabidhi jumla ya pikipiki 50 kwa maafisa ugani kilimo wa BBT Korosho wa wilaya hiyo chini ya Kauli Mbiu Jenga Kesho iliyobora kupitia zao la korosho ambapo vijana hao watakajikita kwenye uzalishaji na ubora wa zao la korosho kuanzia msimu wa mwaka 2025/2026.
Amesema,ni matumaini ya Wilaya hiyo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kuwa,watazalisha kwa wingi kutokana na wataalamu wa kilimo kuwezeshwa vitendea kazi ambavyo vitasaidia kuwafikia wakulima wengi katika Wilaya hiyo.
Masanja,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwapatia vyombo hivyo ambavyo vitakwenda kuinua utendaji kazi wa maafisa hao na kuongeza ubora wa zao la korosho ambalo ni uti wa mgongo kwa wananchi wengi wa Tunduru.
“leo tunashuhudia namna mama yetu Rais Samia anavyo wajali watendaji na wakulima wake,sitegemei pikipiki hizi mkafanyie bodo boda au kufanyia uharifu wowote,nawaomba sana mzitunze na mkafanyie kazi iliyokusudiwa”alisema Dc Masanja.
Amewapongeza maafisa ugani kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwasaidia wakulima wa korosho, ambayo ni muhimu katika kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo ambalo ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa Wilaya ya Tunduru na Mkoa wa Ruvuma.
“Leo tunashuhudia hatua kubwa katika kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima wetu,pikipiki hizi 50 zitawawezesha maafisa ugani kufika kwa urahisi zaidi kwa wakulima,kutoa elimu,ushauri na kufuatilia utekelezaji wa mbinu bora za kilimo”alisema.
Aliongeza kuwa,Serikali ya Mkoa inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo katika maendeleo ya uchumi wetu ndiyo maana inaendelea kuwekeza nguvu kubwa zikiwemo kuboresha huduma za ugani,miundombinu na upatikanaji wa pembejeo bora.
Aidha,amewataka maafisa ugani kuzitumia pikipiki hizo kwa ufanisi na kuhakikisha zinawanufaisha wakulima wote na kufanya kazi kwa bidii,weledi na uwajibikaji ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya korosho.
Kwa mujibu wa Masanja,uwepo wa pikipiki hizo utawezesha kufikiwa lengo la Serikali la uzalishaji wa tani 700,000 za korosho kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi yam waka 2020.
Amewasihi wakulima,kutumia fursa hiyo kupata elimu na ushauri kutoka kwa maafisa ugani hao na kutumia mbinu bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa korosho na Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika sekta ya korosho ili kufikia malengo kwa kuongeza tija,uzalishaji na ubora wa zao hilo.
Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania Tawi la Tunduru Shauri Makiwa alisema,maafisa ugani kilimo wa BBT Korosho ni program maalum inayolenga kuwawezesha vijana ambao ni wataalam wa kilimo kuongeza uzalishaji wa korosho.
Alisema,Wilaya ya Tunduru imepata maafisa ugani 50 ambao wamepelekwa katika kata zote za Wilaya hiyo na kazi kubwa wanayotakiwa kwenda kuifanya ni kuhakikisha zao la korosho linakuwa endelevu kwa kutatua changamoto za wakulima wa zao hilo.
Alisema,tangu kuanzishwa kwa mpango huo changamoto nyingi zimetatuliwa hasa kipindi hiki cha ugawaji na matumizi sahihi ya viuatilifu kwenye zao la korosho ikilinganisha na msimu uliopita.
“katika mkataba wao tuliwahaidi kuwapatia vishikwambi na pikipiki ili kurahisisha kuwafikia wakulima kwa urahisi zaidi na pikipiki hizi zinakwenda kuboresha utendaji kazi kwa maafisa ugani,kuwafikia wakulima kwa urahisi na kuongeza uzalishaji wa zao la korosho”alisema Mokiwa.
Mokiwa,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaofanya katika Mkoa wa Ruvuma hususani katika sekta mama ya kilimo kwa kutoa vitendea kazi na pembejeo za kilimo salfa na dawa za kuuwa wadudu wa korosho.
Mmoja wa vijana waliopatiwa pikipiki Pascal Kaguo alisema,hilo ni jambo kubwa katika sekta ya korosho kwani maafisa ugani walikuwa wamesahaulika,hivyo pikipiki hizo zimejibu kilio chao cha muda mrefu na kazi inayokwenda itakuwa na matokeo makubwa.