Tunduru-Ruvuma.
Serikali Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma, imetangaza rasmi kuanza operesheni kabambe ya kuwaondoa wafugaji wote waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo na uhifadhi,kama hatua ya kudhibiti migogoro inayotokea mara kwa mara kati yao na wakulima.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Denis Masanja, alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Cheleweni kata ya Sisi kwa Sisi wakati wa ziara ya kusikiliza kero na kujitambulisha kwa wananchi inayoendelea katika vijiji mbalimbali.
“kuanzia tarehe 21,tutaanza operesheni ya kuwaondoa wafugaji wote wasiotaka kufuata sheria na kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya kilimo, baada ya zoezi hilo wafugaji watatakiwa kufika kwenye ofisi za Serikali za vijiji ili kuelekezwa maeneo wanayotakiwa kwenda ”alisema Masanja.
Aidha alisema, ili kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji Serikali itaunda kamati ya pamoja itakayohusisha wafugaji, wakulima na baadhi ya wananchi watakaopendelezwa na vijiji husika ambayo itakuwa na jukumu la kutafuta namna ya kuzuia muingiliano kati ya makundi hayo ikiwani mkakati wa Serikali Wilayani humo kukomesha migogoro hiyo.
Alisema,sehemu kubwa ya migogoro inayotokea kati ya wafugaji na wakulima inachangiwa na viongozi wa vijiji na baadhi ya wananchi wanaopokea fedha kutoka kwa wafugaji kwa maslahi binafsi na kuwakaribisha kwenye maeneo ambayo hayatengwa kwa shughuli za ufugaji.
Dc Masanja,amewataka wananchi kuacha tabia ya kuwakaribisha wafugaji na watu wasiowafahamu bila kufuata sheria kwa kuwa tabia hiyo inachochea sana kuwepo na kuongezeka kwa migogoro kati ya makundi hayo mawili.
Katika hatua nyingine,Masanja amehaidi kufanyia kazi changamoto ya barabara inayoanzia katika kijiji hicho hadi makao makuu ya kata Sisi kwa Sisi iliyoharibika vibaya na mvua za masika ili huduma ya usafiri na usafirishaji ziweze kujerea kama kawaida.
Masanja,amewaomba wananchi wa kijiji hicho kuwa na tabia ya kushirikiana na Serikali katika ujenzi na kutunza miradi ya maendeleo inayojengwa kwa fedha nyingi ikiwemo vyumba vya madarasa badala ya kuichia Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Tunduru Chiza Marando alisema,jumla ya vitalu 221 vimetengwa kwa ajili ya wafugaji katika maeneo mbalimbali na amewataka wafugaji kwenda kwenye maeneo yao ili kuepusha migogoro.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Mustafa Ponera alisema,kutokana na ubovu wa barabara hiyo kwa sasa wananchi wanalazimika kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa 7 hadi kijiji jirani cha Sisi kwa Sisi ili kupanda magari wanapotaka kwenda Tunduru mjini kufuata huduma za kijamii.
Alisema,wamiliki wa magari wamesitisha kupeleka magari yao katika kijiji hicho kwa kuhofia kuharibika kutokana na ubovu wa barabara inayounganisha kijiji hicho na maeneo mengine iliyoharibika vibaya kutokana na mvua za masika.
Meneja wa Tarura Wilayani Tunduru Silvanus Ngonyani alisema,Serikali imetenga kiasi cha Sh.milioni 155 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara katika kata ya Sisi kwa Sisi.
“kabla ya mwezi wa nane barabara zote zenye changamoto zitafanyiwa kazi,nawaomba wananchi kuwa wavumilivu kwani Serikali yao inatambua changamoto iliyopo na itazifanyia kazi”alisema.