Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wa Tarafa ya Bungu iliyopo Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga wamempongeza Afisa Tarafa wa hiyo Peter Kahindi kwa juhudi zake za uratibu wa masuala mbalimbali ya Kiserikali na kijamii ndani ya Kata hiyo na Wilaya kwa ujumla.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kumalizika kwa kambi ya afya iloyofanyika katika Tarafa hiyo, wakazi hao wamesema tangu aingie katika Kata hiyo Afisa Tarafa huyo amekuwa chachu kwa wao wananchi kujiletea maendeleo.
Wamesema bila kujali umri wake mdogo, Kahindi amekuwa akishirikiana vyema na wakazi wa Tarafa hiyo ikiwa ni pamoja na kuwahusisha wazee katika mambo mengi yanayohusu maendeleo jambo linalowafanya wakubali uwezo wake.
“Ukweli tangu ameanza kazi katika Kata yetu mambo mengi yanaenda vizuri, amekuwa mshauri mzuri katika masuala mengi bila kuangalia huyu nani na huyu nani, hakika ameonesha mfano hai wa viongozi wanaofanya kazi nzuri katika kumsaidia Rais wetu Samia Suluhu Hassan” alisema mmoja wa wakazi wa Tarafa hiyo.
Aidha akizungumzia kuhusu kambi ya Afya ya ‘Samia Afya Check’ iliyofanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 17 hadi 19, Mkazi huyo mbali na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha upendo wake kwao, alimpongeza Afisa Tarafa huyo kwa usimamizi wake Hadi zoezi hilo lilipokamilika.
” Tunamshukuru sana Mama na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kupata kambi hii ya Afya, imetuwezesha kuchunguzwa afya zetu na kujua Hali tuliyonayo, hakika hili kwetu ni deni na tutahakikisha Oktoba Tunatiki ili aweze kuendeleza yale yote mazuri aliyokuwa akiyafanya” amesisitiza mkazi huyo.
Naye mwananchi mwingine aitwaye Mussa amesema kupitia kanbi hiyo ya ‘Samia Afya Check’ wao kama wakazi wa Kata hiyo wanaamini juhudi za Afisa Tarafa huyo ndiyo zimewezesha kwa kambi hiyo kufanyika kutokana na ushirikiano wake mzuri alionao na viongozi wenzake kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya Mkoa hadi Taifa.
Amesema kwa kipindi kifupi tangu amfahamu Afisa Tarafa huyo, amekuwa na imani juu yake kwa kiasi kikubwa huku akiwataka wananchi wenzake kuendelea kumpa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutimiza majukumu yake ya kusimamia shughuli mbalimbali katika Kata hiyo.
Amesisitiza kuwa imani yake kama wananchi wataendelea kumuamini na kumpa ushirikiano huo, historia ya Kata ya Bungu itaendelea kujijenga upya siku hadi siku kutokana na kazi anazofanya Kiongozi huyo kuendana na kasi ile ile inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.