Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Taasisi ya WIOMSA(West Indian Ocean Marine Science Association) wanaendesha Warsha kwa wadau wa Sekta mbalimbali za Serikali, binafsi na Sekta za kijamii kuhusu mchango wa vyakula vya baharini, mitoni na maziwa “Blue foods” katika lishe na usalama wa chakula.
Warsha hiyo ya Siku mbili inafanyika kuanzia leo tarehe 21 hadi 22 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Hoteli ya Tanga Resort Mkoani Tanga.
Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha hiyo Mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa buluu na Uvuvi Zanzibar Mhe. Zahor Kassim Mohamed ameeleza kuwa vyakula vya buluu “Blue foods” ni muhimu sana katika lishe bora na usalama wa chakula.
“Vyakula vya buluu “Blue foods” kama vile samaki, dagaa, kaa, majongoo wa baharini, mwani na viumbe wengine vinamchango mkubwa katika lishe bora, usalama wa chakula, uchumi wa Kaya na ajira.” Amesema Mhe. Zahor Mohamed.
Akiongea na Waandishi wa habari mara baada ya awamu ya kwanza ya Warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema lengo kuu la Warsha hii ni kuhamasisha juu ya umuhimu wa vyakula vya baharini, katika mito na maziwa “Blue foods” katika lishe bora kwani vyakula hivyo vinamanufaa makubwa katika Afya ya mwanadamu na hivyo kujenga Taifa lenye watu wenye uelewa na kuweza kujitegemea.
Akiwasilisha mada Mkurugenzi wa Taasisi ya WIOMSA Dkt. Arthur Tude amesema Taasisi hiyo imejikita katika tafiti za kuboresha lishe bora na kuelimisha jamii kuhusu vyakula vya baharini, hivyo imeamua kushirikiana na NEMC Pamoja na Taasisi nyinginezo kuhamasisha jamii juu ya uvunaji wa vyakula vya baharini vyenye lishe bora.
Aidha, Zahor alisisitiza kuwa ni muhimu Sekta zote binafsi na za Serikali, Taasisi na washirika wa maendeleo na jamii za uvuvi kuhakikisha kuwa “blue food” zinachangia kwa ufanisi kutokomeza njaa, kuongeza kipato na kulinda Mazingira ya bahari, mito na maziwa ambavyo ni rasilimali muhimu za kufuga vyakula buluu.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto zinazokabili ustawi wa vyakula vya buluu, Serikali imeweza kuimarisha Sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuwezesha ufugaji samaki katika mabwawa ya kisasa, kuwezesha vikundi vya Wanawake na vijana katika mnyororo wa thamani wa mazao ya maji, kushiriki katika juhudi za kimataifa za na kikanda kama vile Blue Economy na mabadiliko ya mifumo ya chakula duniani.