Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia, wametangaza kuanza rasmi kwa shindano la uandishi
wa insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho
ya kumbukizi ya miaka 26 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Huduma za Televisheni wa TBC, Bi. Happiness Ngasala, amesema
shindano hilo lina lengo la kuwahamasisha vijana kuenzi mchango wa Mwalimu
Nyerere kwa njia ya maandishi na tafakuri ya kina kuhusu juhudi zake katika
kulijenga taifa.
“Tunataka wanafunzi waandike insha zitakazoonyesha uelewa
wao kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere katika mapambano dhidi ya ujinga, maradhi
na umasikini,” amesema Bi. Ngasala.
Shindano hili litahusisha wanafunzi wote kuanzia kidato cha
kwanza hadi cha sita, likiwa na mada kuu zinazolenga kuangazia falsafa ya
Mwalimu Nyerere na maono yake katika maendeleo ya taifa. Lugha zitakazotumika
ni Kiswahili na Kiingereza, na washindi watano bora watazawadiwa kompyuta mpakato
na fedha taslimu.
Aidha, Bi. Ngasala amebainisha kuwa kutakuwa na uchunguzi
maalum wa kuhakikisha uhalisia wa kazi zinazowasilishwa, huku akionya kuwa
matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) kughushi insha ni kosa
litakalosababisha mshiriki kuondolewa kwenye shindano.
Shindano limezinduliwa leo, Julai 22, 2025, na
litahitimishwa rasmi Oktoba 14, 2025 – siku ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu
Nyerere. Kilele cha maadhimisho hayo kitasindikizwa na mbio za pole za “Mwalimu
Nyerere Marathon.”
Wanafunzi wa shule zote za sekondari nchini wanahimizwa
kushiriki kwa wingi ili kuenzi urithi wa Baba wa Taifa. Utaratibu rasmi wa
ushiriki utatangazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ya TBC na
Wizara husika.