Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni miongoni mwa Watu Mashuhuri (Eminent Persons) kutoka bara la Afrika walioshiriki katika Kongamano Maalumu kuhusu Maendeleo, Usalama wa Chakula na Uchumi Endelevu wa Bluu barani Afrika lililofanyika tarehe 23 – 24, Julai 2025 katika mji wa Hakone, Japan.
Kongamano hilo lililoandaliwa kwa pamoja na Taasisi za Sasakawa Peace Foundation na Nippon Foundation za Japan limelenga kujadili na kutoa mapendekezo ya kisera kwa Serikali ya Japan katika kuandaa mikakati ya ushirikiano wake na nchi za bara la Afrika katika maeneo ya usalama wa chakula na uchumi endelevu wa bluu.
Mawazo na mapendekezo hayo yanatarajiwa kushawishi uandaaji wa ajenda za Mkutano wa Kimataifa wa 9 wa Tokyo kuhusu Maendeleo kwa Bara la Afrika (TICAD 9) utakaofanyika jijini Tokyo, Japan tarehe 20 – 22 mwezi Agosti 2025.
Viongozi wengine mashuhuri walioshiriki Kongamano hilo ni Jorge Carlos Fonseca, Rais Mstaafu wa Cabo Verde, Ibrahim Hassane Mayaki, Waziri Mkuu Mstaafu wa Niger, ambaye pia ni Mjumbe Maalumu wa Mifumo ya Chakula wa Umoja wa Afrika na Dkt. Donald Kaberuka, Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayetokea Rwanda. Wengine ni Mzee Olusegun Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria na Dk. Geraldine Fraser-Moloketi, Waziri Mstaafu wa aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Afrika Kusini.
Kwa upande wa Japan, Kongamano hilo limehudhuriwa na Mwenyekiti wa Heshima wa Taasisi ya Nippon Foundation, Yohei Sasakawa, Rais wa Sasakawa Peace Foundation, Dkt. Atsushi Sunami, Mwenyekiti wa Sasakawa Africa Association, Dkt. Amit Roy pamoja na Masanori Kobayashi, ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Sasakawa Peace Foundation.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kikwete ametumia fursa ya kushiriki Kongamano hilo kuelezea hatua zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha mifumo na usalama wa chakula nchini Tanzania, hususan katika eneo la uvuvi.
Vilevile, ametoa mapendekezo ya namna ya kuboresha ushirikiano kati ya Japan na bara la Afrika, hususan kwa nchi zinazofanya shughuli za kiuchumi kupitia fukwe za bahari, maziwa na mito kama vile Tanzania.
Aidha, ameainisha fursa za ushirikiano zilizopo baina ya pande hizo mbili katika kuendeleza utafiti na kukuza matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza tija ya uvuvi mdogo mdogo na ufugaji wa samani kote nchini, pamoja na kukuza zaidi kilimo cha mwani, hususan kwa upande wa Zanzibar.
Yohei Sasakawa, Mwenyekiti wa Heshima wa Nippon Foundation akichangia jambo
Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza Kongamano Maalumu kuhusu Maendeleo, Usalama wa Chakula na Uchumi Endelevu wa Bluu barani Afrika lililofanyika tarehe 23 – 24, Julai 2025 katika mji wa Hakone, Japan.