Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Masonya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwajengea bweni la chakula litakalowaondolea adha ya kula chakula chini ya miti.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Marian Michael alisema bweni hilo litakuwa msaada mkubwa kwao kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakila chakula chini ya miti na wengine madarasani jambo linalohatarisha afya zao.
Ameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa bweni hilo, ili waweze kuondokana na kero hiyo baada ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi hasa wa kidato cha tano katika muhula wa masomo 2025/2026.
Mkuu wa shule hiyo, Makrina Ngonyani alisema, ujenzi wa bwalo la chakula ulianza mwezi Juni kwa kusafisha eneo la ujenzi na kazi ya ujenzi imeanza kwa kujaza kifusi kwenye msingi ili hatua za upangaji wa mawe kabla ya kumwaga zege na litagharimu zaidi ya Sh. milioni 168.
Alisema, hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh. milioni 102,744,500.00 na zilizobaki ni Sh. milioni 65,255,500.00 lakini changamoto iliyopo ni kuongezeka kwa gharama za ujenzi kutojumuishwa kwenye makadirio ya vifaa na ufundi hivyo kufanya ugumu katika utekelezaji wa mradi huo.
Ngonyani ametaja gharama hizo ni maji, kusafisha eneo na ziada ya vifaa inayotokana na mteremko wa eneo la mradi unapotekelezwa jambo linalopelekea gharama za mradi kuongezeka na hesabu ya utekelezaji wa mradi kubadilika ikilinganishwa na mwongozo.
Aidha alisema, katika kipindi cha miaka mitatu shule hiyo imepokea miradi ya ujenzi wa miundombinu ambayo imeleta mabadiliko na muonekano mpya na kuvutia katika Shule ya Sekondari Masonya.
Ametaja miradi hiyo ni ujenzi wa mabweni manne, madarasa kumi na matundu ya vyoo kumi na tano iliyogharimu Sh. milioni 775 na ujenzi wa bweni moja kupitia mradi wa Sequip kwa gharama ya Sh. milioni 128.
“Mhehimiwa Mkuu wa Wilaya, katika kipindi cha miaka mitatu miradi mingine tuliyotekeleza ni ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu ya vyoo kumi na tano kwa gharama ya Sh. milioni 121,” alisema Ngonyani.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ambayo imebadili sura ya shule hiyo na kuonekana kuwa mpya licha ya kuwa ya zamani.
Alisema, bwalo hilo linakwenda kumaliza kiu ya jamii kwa kurahisisha mambo mengi ikiwemo vikao, mikutano na mitihani mbalimbali ambayo itafanyika katika ukumbi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, amewataka mafundi kuongeza kasi ya ujenzi kwa bwalo hilo ili likamilike na wanafunzi wapate sehemu ya kulia chakula kabla ya mvua za masika hazijaanza kunyesha.
Masanja, amewapongeza walimu kwa usimamizi mzuri wa fedha na miradi inayotekelezwa pamoja na kazi nzuri ambayo imewezesha wanafunzi waliyo fanya mitihani ya kidato cha sita kupata matokeo mazuri.
Amewaomba kuwa wavumilivu kwenye majukumu yao, kwani Serikali inaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi, kuwa na upendo kwa wanafunzi na kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa.