NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Tanzania imeendelea kuonesha uongozi bora katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kusimamia kwa mafanikio masuala ya siasa, ulinzi na usalama ndani ya ukanda huo, ikiwa ni miezi kumi tangu ichukue nafasi ya Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Kombo wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Mawaziri wa Kamati ya Asasi hiyo uliofanyika leo Julai 24, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo mawaziri kutoka nchi mbalimbali wanachama wa SADC walihudhuria.
“Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha maamuzi ya vikao vya juu yanatekelezwa kwa ufanisi. Takribani asilimia 70 ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri wa Asasi yaliyofikiwa katika mkutano wa 27 yametekelezwa,” amesema Balozi Kombo.
Aidha amesema zaidi ya asilimia 70 ya maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa 27 wa Mawaziri wa Asasi hiyo yamefanikiwa kutekelezwa, ikiwa ni ishara ya mafanikio ya ushirikiano na ufuatiliaji madhubuti kati ya Sekretarieti ya SADC na nchi wanachama.
Amesema kuwa Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba 2025 na imefungua milango kwa waangalizi wa uchaguzi kutoka SADC kufuatilia mchakato huo kwa ukaribu, huku ikiahidi kuwa uchaguzi huo utaendeshwa kwa misingi ya haki, uhuru na amani.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwatakia mafanikio Malawi na Shelisheli ambazo zinatarajia kufanya chaguzi zao mwezi Septemba 2025.
Amesema katika usalama wa umma, nchi wanachama ziko kwenye mkondo mzuri wa kuruhusu uhuru wa watu kusafiri, kushughulikia uhalifu wa kimataifa na biashara haramu ya silaha ndogo.
Katika kupambana na rushwa, amesema kuwa nchi wanachama zimeendelea kutekeleza Mpango wa SADC wa Kupambana na Rushwa na zimeanza kutumia mbinu mpya kama vile kuanzisha Kiashiria cha Kikanda cha Juhudi Dhidi ya Rushwa ambapo nchi mbili Mauritius na Tanzania tayari zimeanza majaribio.