Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) leo Julai 25, 2025, wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitano kuanzia tarehe 25 Julai 2025 hadi 24 Julai 2030.
Makubaliano hayo ni muendelezo wa ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi hizo mbili ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha wataalamu wa kodi, wanachama, wanataaluma, wanafunzi na wadau wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi, pamoja na wapenda maendeleo wengine, kuhusu umuhimu wa ukusanyaji wa kodi kwa maendeleo ya Taifa, usimamizi bora wa kodi, viwango vya uandaaji wa hesabu na mbinu bora za ukaguzi wa hesabu.
Hafla ya utiaji saini imefanyika Makao Makuu ya TRA jijini Dar es Salaam na kuhusisha viongozi wakuu wa taasisi hizo. Hati hiyo imesainiwa na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno.
Akizungumza katika hafla hiyo, CPA Yusufu Juma Mwenda alieleza kuwa ushirikiano huu utaimarisha zaidi ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kuunganisha nguvu na maarifa ya wataalamu wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi nchini. Alisisitiza kuwa TRA itaendelea kushirikiana kwa karibu na NBAA ili kuhakikisha kwamba taarifa za kifedha zinazingatia viwango sahihi vya kitaalamu, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika masuala ya kikodi.
Naye CPA Pius Maneno, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, alisema kuwa makubaliano hayo yamekuja katika wakati muafaka ambapo taasisi hiyo imezindua mfumo mpya wa kiteknolojia uitwao NBAAVN, ambao utasaidia kutambua taarifa halali za hesabu kwa kuwapatia namba maalumu ya utambuzi, hivyo kukomesha matumizi ya wahasibu vishoka. Aliongeza kuwa mfumo huo utarahisisha usomaji wa taarifa kati ya NBAA na TRA, hatua ambayo ni muhimu katika kuhakikisha ufanisi wa pamoja.
Makubaliano hayo yana nafasi ya kuendelezwa au kuongezewa muda pindi yatakapofikia ukomo. Hatua hii ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za umma, kwa kuwa inaonyesha namna ambavyo ushirikiano wa karibu unaweza kuongeza tija katika utoaji wa huduma na kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya Taifa.
Itakumbukwa kuwa hii ni hati ya pili ya makubaliano kusainiwa na NBAA ndani ya mwaka huu, baada ya ile ya tarehe 16 Mei 2025 kati ya NBAA na Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri wa Kodi Zanzibar (ZIAAT), ambayo pia inalenga kuendeleza taaluma ya uhasibu na ushauri wa kodi nchini.
Makubaliano hayo pia ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana kwa karibu, kubadilishana taarifa na kutumia teknolojia katika kuongeza uwazi, ufanisi na mapato ya Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (kushoto) pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda (kulia) wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa sambamba na kusomana kwa mifumo kati ya taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (kushoto) pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda (kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano ya upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa sambamba na kusomana kwa mifumo kati ya taasisi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno (kushoto) pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda (kulia) wakibadilishana hati ya makubaliano ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano hayo katika ofisi za TRA Makao Makuu jijini Dar es Salaam
Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za kikodi na kihesabu ikiwa sambamba na kusomana kwa mifumo kati ya taasisi hizo mbili.
Mkutano ukiendelea
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusufu Juma Mwenda wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NBAA na TRA mara baada ya kusaini hati ya makubaliano ya upatikaji wa taarifa mbalimbali kati ya taasisi hizo mbili