Na Pamela Mollel, Arusha
Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 5.5 mwaka 2024, hali inayoonesha mwelekeo mzuri wa maendeleo ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa Julai 24, 2024 jijini Arusha na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe Deus Clement Sangu (Mb), wakati akifunga rasmi Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Jumuiya ya Wataalamu wa Usimamizi wa Rasilimaliwatu na Utawala (TAPA-HR).
Naibu Waziri Sangu alisema kuwa jitihada kubwa za serikali zimewezesha uchumi kuendelea kuimarika, na akasisitiza kuwa wataalamu wa rasilimali watu wana mchango mkubwa katika kuhakikisha watumishi wa umma wanasimamiwa ipasavyo kwa maendeleo ya taifa.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri ya kusimamia watumishi wa umma, tumeona mabadiliko makubwa, lakini niwakumbushe kuwa kutowajibika kikamilifu kunaweza kuisababishia serikali hasara kubwa, alisema Sangu.
Akitoa mfano, alieleza tukio la mwaka 2016 ambapo taasisi moja ya umma ilifukuza watumishi 40 bila kufuata taratibu, na baada ya kukata rufaa, mahakama iliamuru warejeshwe kazini na walipwe zaidi ya shilingi bilioni 40.
“Mtumishi mmoja anatakiwa alipwe zaidi ya bilioni moja, haya ni madhara ya mtu mmoja kutowajibika kazini, na sasa serikali inalazimika kulipa madeni badala ya kuendelea na miradi ya maendeleo, aliongeza Naibu Waziri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAPA-HR, Bi. Grace Meshy, aliipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka sera bora zinazoboresha mazingira ya kazi na motisha kwa watumishi wa umma.
“Tunashukuru serikali kwa jitihada zake katika kuboresha sekta ya utumishi,tumeshuhudia mazingira bora ya kazi na ushirikiano mzuri baina ya serikali na wataalamu wa sekta hii, alisema Bi. Meshy.
Aidha, aliwapongeza waajiri kwa kuruhusu zaidi ya washiriki 1,000 kuhudhuria mkutano huo, hatua inayoonesha kuthamini taaluma ya usimamizi wa rasilimali watu nchini.