Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imevitaka Vyama vya siasa na wafuasi wake kuendesha kampeni kwa uvumilivu na staha ili kulinda amani na mshikamano wa taifa.
Hayo yameelezwa leo Julai 27,2025 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo,Jaji Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa Kitaifa wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na Vyama vya siasa kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wa juu wa vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo akiwemo Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Prof Ibrahim Lipumba,Mwenyekiti wa Chaumma,Hashim Rungwe na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Addo Shaibu.
“Kipindi cha kampeni mara nyingi huambatana na joto la kisiasa kutokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu. Tume inawasihi viongozi wa vyama na wafuasi wao kufanya kampeni za kistaarabu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi,” amesema NEC.
Mwenyekiti huyo amesema maandalizi na usimamizi wa kampeni yanazingatia usawa, amani na mshikamano wa kitaifa.
Aida Jaji Mwambegele amesisitiza imesisitiza kuhakikisha kunakuwa na uwanja sawa kwa vyama vyote vya siasa, ambapo ratiba za kampeni zitapangwa na kuratibiwa na kamati husika katika ngazi mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Tume, Ramadhani Kailima, ameeleza kuwa maandalizi maalum yanaendelea ili kuhakikisha kuwa mahabusu na wafungwa wanaotimiza vigezo vya kisheria wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.
“Tunajipanga kuhakikisha kuwa haki ya kila Mtanzania, wakiwemo wafungwa na mahabusu, inalindwa. Utaratibu wa kuwahusisha katika upigaji kura uko katika hatua nzuri ya maandalizi,” amesema Kailima.
Mkutano huo wa siku moja unashirikisha viongozi wa vyama vya siasa, maafisa wa uchaguzi na wadau mbalimbali wa demokrasia, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa kihistoria utakaofanyika mwaka 2025.