
Klabu ya Singida Black Stars imethibitisha rasmi kuondoka kwa mshambuliaji wao nyota, Jonathan Sowah, raia wa Ghana, ambaye amejiunga na Simba SC kwa uhamisho wa kudumu.
Kupitia taarifa yao kwa umma, Singida Black Stars imesema kuwa makubaliano ya uhamisho huo yamefikiwa kwa msingi wa mashauriano na makubaliano maalum kati ya Mlezi wa klabu hiyo, Rais wa Heshima wa Simba SC, pamoja na uongozi wa pande zote mbili.
“Uongozi wa Singida BS unawataarifu mashabiki, wapenzi na wadau wote wa soka kuwa umeridhia Simba SC kumsajili mchezaji wetu tegemeo, Jonathan Sowah, kwa uhamisho wa kudumu kwa MAKUBALIANO MAALUM,” imesema taarifa hiyo.
Aidha, klabu hiyo imemshukuru Sowah kwa mchango wake ndani ya kikosi hicho na kumtakia mafanikio katika changamoto mpya.
“Tunamtakia Jonathan Sowah kila la heri katika changamoto mpya na tunamshukuru kwa kuitumikia vyema klabu yetu katika kipindi chote alichokuwa nasi.”
Jonathan Sowah alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Singida Black Stars na mchango wake ulichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya klabu hiyo msimu uliopita.