Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Profesa Tumaini Nagu, amewaomba viongozi wa Sekta ya Afya nchini kutokuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa watumishi katika maeneo ya kazi.
Profesa Nagu ametoa wito huo kwenye kikao cha majumuisho ya usimamizi shirikishi mkoani Tanga, ambapo kikao hicho kimehudhuriwa na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Tanga, baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga kama mgeni rasmi.
“Viongozi tusiwa sehemu ya msongo wa mawazo kwa watumishi wetu sisi tuwe sehemu ya ‘team building’ viongozi tunatakiwa kuelewa ‘strength’ na ‘weakness’ wa watumishi na kuwafanyia ‘mentorship’ ili zile strength’ ziongezeke na ‘weakness’ zipungue.” Amesema
Katika kikao hicho, Profesa Nagu amesisitiza kuwa ni muhimu kwa viongozi kutoa muongozo wa mara kwa mara ili kuimarisha uwezo kwa watumishi na kuondoa baadhi ya mapungufu yanayoweza kujitokeza katika maeneo ya kutolea huduma za afya na kuathiri wateja.
Aidha, Profesa Nagu amewapongeza watumishi wa Sekta ya Afya kwa uwajibikaji wao na moyo wa kujitolea katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Muda mwingi tunatumia kwenye kazi kwa kweli niwapongeze sana watumishi hasa sekta ya Afya na watumishi wa serikali kwa ujumla tunatumia muda mwingi kufanyakazi na mnafanya kazi kwa bidii.” Amesema
Profesa Nagu, amehitimisha ziara ya usimamizi shirikishi katika Mkoa wa Tanga ambapo ameelekeza usimamizi wa fedha, ukamilishwaji wa majengo ya kutolea huduma za afya na kuwahamasisha wananchi kujiunga Bima ya Afya kwa wote.