Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Julai 28, 2025
Alhaj Abubakar Kunenge, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ametoa msisitizo kwa Manispaa ya Mji wa Kibaha pamoja na halmashauri mkoani humo, kuhakikisha zinazingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), na Mpango wa Taifa wa Maendeleo katika kuainisha vipaumbele vyao.
Msisitizo huo aliutoa Julai 27, 2025, wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kuhusu tathmini ya utekelezaji wa mipango na uendeshaji wa fedha kwa mwaka 2024/2025 na muelekeo wa mwaka mpya wa fedha 2025/2026 kwa watumishi 600 wa Manispaa ya Mji wa Kibaha yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha kwa Mfipa.
Kunenge alieleza, haitarajii kuona Manispaa ama Halmashauri zikiweka vipaumbele ambavyo havijajikita katika dira ya taifa, mpango wa maendeleo, na utekelezaji wa ilani ya Chama Tawala .
Aidha, alieleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajia changamoto na kero za wananchi zitatatuliwa kuanzia ngazi za chini.
Alifafanua, haipendezi wananchi kukimbilia ngazi za juu kuomba msaada wakati wapo viongozi, watendaji na watumishi wa umma walioko karibu nao wenye uwezo wa kushughulikia matatizo hayo.
Vilevile Kunenge aliwasihi watumishi na watendaji wa Manispaa hiyo kufanya kazi kwa mshikamano, kila mmoja akitimiza wajibu wake kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, alieleza ,mwaka wa fedha 2024 /2025 walikusanya kiasi cha sh. bilioni 8 ambapo kwa mwaka 2025/2026 wamelenga kukusanya bilioni 13.865 lakini malengo yao ni kukusanya kiasi cha sh. bilioni 20.
“Kwa sasa Manispaa imejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati itakayochochea maendeleo ya kiuchumi na kupunguza utegemezi, ikiwemo ujenzi wa kituo cha mafuta, kituo cha biashara, na maegesho ya kisasa ya magari,” alieleza Shemwelekwa.
Shemwelekwa alitaja miradi mingine, kuwa ni ukarabati wa barabara za ndani kwa sh. milioni 520, uanzishaji wa shamba darasa eneo la Mitamba kwa milioni 60, pamoja na milioni 247 kwa ajili ya ununuzi wa laptop na vishkwambi kwa watumishi.
Alisema pia Manispaa hiyo imetenga zaidi ya Shilingi bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa magari sita, yakiwemo maroli mawili, pickup mbili na basi dogo aina ya coaster, ambapo tayari wameshapata kibali cha manunuzi hayo.
“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini na kutuwezesha fedha za miradi. Kama watumishi, tumejipanga kuhakikisha tunampatia Rais furaha mwezi Oktoba,” aliongeza Shemwelekwa.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Mtendaji wa Kata ya Viziwaziwa, Francis Shao, na Mtendaji wa Kata ya Tumbi, Msemakweli Kalia, walisema mafunzo hayo yamekuwa ya tija na yamewaongezea uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Bahati Anatory, Mhasibu wa Manispaa ya Kibaha Mjini, pamoja na Godfrey Ntandu, walimshukuru Mkurugenzi Shemwelekwa kwa kuandaa mafunzo hayo, wakisema yatasaidia kuboresha maadili, uwajibikaji na ufanisi kazini.