Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika juhudi za kimataifa za mageuzi ya mifumo ya chakula duniani, ikilenga kujenga mifumo endelevu, jumuishi na yenye ustahimilivu kwa ajili ya ustawi wa watu, sayari na uchumi wa dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, ametoa kauli hiyo alipowasilisha tamko la Tanzania katika kikao cha Mkutano wa Pili wa Mfumo wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (UNFSS+4), unaofanyika jijini Addis Ababa kuanzia tarehe 27 hadi 29 Julai 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Kombo ameeleza kuwa licha ya changamoto nyingi za kimataifa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya kiuchumi na ukosefu wa usawa, Tanzania inaendelea kutekeleza mkakati wake wa mageuzi ya mifumo ya chakula kwa kuzingatia misingi ya usawa wa kijinsia, utawala bora na maendeleo shirikishi.
“Chakula lazima kisiishie kutulisha tu, bali kiwe sehemu ya kuimarisha uchumi wetu, kurejesha mazingira yetu na kulinda heshima ya kila mwanadamu,” alisema Waziri Kombo, akisisitiza kwamba Tanzania inajielekeza katika kilimo rafiki kwa mazingira, uwezeshaji wa wakulima wadogo, wanawake na vijana, pamoja na kuunganisha lishe bora katika sera na mipango ya kitaifa.
Katika hotuba hiyo, Tanzania pia imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha mshikamano, kuongeza uwekezaji katika kilimo endelevu, na kutoa teknolojia na rasilimali ili kuongeza ushiriki wao katika mifumo ya chakula ya dunia.
Mkutano wa UNFSS+4 ni jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio na changamoto zilizojitokeza tangu mkutano wa awali wa mwaka 2021, huku ukilenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kupatikana kwa mifumo ya chakula salama, shirikishi na inayojali mazingira.