
Niger State, Nigeria – Takriban watu 13 wamethibitishwa kufariki dunia baada ya boti iliyokuwa imebeba abiria na mizigo kuzama Jumapili katika mto ulioko karibu na soko maarufu la Zumba, Kaskazini mwa Nigeria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Taifa la Kukabiliana na Dharura (NEMA) kupitia ukurasa wao wa X (zamani Twitter), boti hiyo ilikuwa ikisafirisha abiria 39 na magunia 50 ya mchele kuelekea sokoni, kabla ya kupoteza mwelekeo na kuzama katikati ya safari.
Miongoni mwa waliopoteza maisha ni wanawake 8, wanaume 3, na watoto 2. Dereva wa boti na abiria wengine 25 waliokolewa wakiwa hai.
Hata hivyo, juhudi za uokoaji zilikumbwa na changamoto kubwa kutokana na ongezeko la mashambulizi ya magenge ya kihalifu yanayofahamika kama “bandits” katika jimbo hilo. Afisa wa NEMA, Ibrahim Hussaini, aliliambia shirika la habari la AP kuwa maeneo hayo ni hatarishi na wachache waliweza kufika kwenye eneo la tukio.
“Ni watu wachache sana wanaweza kufika kwenye eneo hilo kwa sababu ya matukio ya uhalifu unaoendelea,” alisema Hussaini.
Mnamo Ijumaa, jeshi la Nigeria lilifanya oparesheni kali katika eneo la Shiroro — ambako soko la Zumba linapatikana — na kuwaua wanachama 45 wa magenge hayo. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, jeshi liliingilia kati baada ya kupata taarifa kuwa kundi kubwa la magaidi lilikuwa linapanga kushambulia vijiji kwa kutumia pikipiki.
Ripoti za Amnesty International zinaeleza kuwa magenge haya yamekuwa yakitekeleza mashambulizi ya kutisha kwa miaka kadhaa, wakiwavamia wakazi wa vijiji kwa risasi, kuchoma nyumba, kuiba mifugo na kuwateka nyara watu kwa lengo la kupata fidia.
Tukio hili la kusikitisha limeongeza huzuni miongoni mwa jamii zinazokabiliwa na mfululizo wa migogoro ya kiusalama na majanga ya asili, huku likionyesha namna hatari za usafiri majini zinavyoendelea kuwa tishio kwa maisha ya wananchi wa maeneo ya vijijini.
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV — usisahau ku-like, ku-comment na ku-subscribe ili uendelee kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.