…….
Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamehakikishiwa kuwa Serikali imejenga upya lililokuwa soko dogo na kukarabati soko lililoungua kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi ya Watanzania wote bila ubaguzi.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Abdulkarim leo (28 Julai 2025) katika ukumbi wa soko la Machinga Dar es Salaam wakati alipofanya kikao na wafanyabiashara wa Soko hilo wanaotarajiwa kurejeshwa ndani ya soko.
CPA Abdulkarim alisema lengo la kikao hicho ni kuwapa mrejesho na taarifa juu ya maendeleo ya mradi na hatua zinazofanyika na Shirika kuwapanga wafanyabiashara ndani ya soko.
Ninawaahidi kuwa tutasikiliza kila mfanyabiashara na kutatua changamoto zake kwa mujibu wa sheria na taratibu za upangishaji za Serikali ili kila mtu apate haki yake na kunufaika na uwepo wa soko la Kariakoo, alisema CPA Abdulkarim.
Meneja Mkuu huyo amewasihi wafanyabiashara hao kuwa mabalozi wa soko hilo kwa kuelezea mazuri yanayofanywa na Serikali ili wananchi wanufaike.
Kikao hicho kilihusisha wafanyabiashara wa pembejeo, viuatilifu, mizani, cherehani, vifungashio, nafaka na viungo vikavu ambao wamepangiwa sakafu ya tatu, nne na tano soko jipya huku baadhi yao wakiwa na maoni ya kuboresha mchakato kuelekea ufunguzi wa soko hilo.
Emanuel Mbise, Mwenyekiti wa wauza pembejeo za kilimo alisema Shirika liweke wazi mikataba wa upangishaji pamoja na kutorusu biashara za pembejeo kuchanganywa na bidhaa zingine ili kulinda walaji.
Naye Abdala Bashiru Selemani alitoa rai kwa uongozi wa Shirika kuwapanga waliokuwa wafanyabiashara soko lililoungua ambao sasa watapangiwa soko jipya sakafu ya nne ili wawe na uhakiki wa biashara badala ya kuchanganywa na makundi mengine.
Ashraph Waziri mfanyabiashara ya nafaka aliomba Serikali ifikirie kuwapa muda wa matazamio na nafuu ya kodi wafanyabiashara wote ambao walipata hasara ya mali zao kutekeketea kwenye tukio la moto la 10 Julai 2021 kwa kuwa hakuna fidia yoyote hadi sasa waliopata.
Akijibu hoja na maswali hayo Meneja Mkuu CPA Abdulkarim alisema wataziratibu hoja hizo kuzitafutia majawabu ikiwemo kuongeza nafasi za majadiliano na wafanyabiashara wakati huu wa kuelekea ufunguzi wa Soko la Kariakoo ikiwemo kutoa elimu ya bima ya majanga ikiwemo moto.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa fedha shilingi Bilioni 28.03 ambazo zilifanya kazi ya kujenga soko jipya na kukarabati la zamani hatua inayofanya soko kuwa la kisasa ambapo maeneo ya biashara yameongezeka toka 1,662 mwaka 2021 hadi 1,907 na ajira zaidi ya 4,000 zitazalishwa.