Kibaha, Pwani. Watendaji wakuu wa taasisi za umma wamepatiwa maagizo sita (6) yenye lengo la kuongeza ufanisi wa taasisi wanazoziongoza na hivyo kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikali kuu.
Maagizo hayo yaliyotolewa Jumatatu, Julai 28, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi. Dk. Moses Kusiluka na na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija, pamoja na Kujenga uwezo wa ndani wa taasisi kwa kuboresha rasilimali watu, teknolojia na miundombinu.
Maagizo mengine ni kuongeza faida kwa taasisi za kibiashara, kuboresha huduma kwa taasisi za huduma, Kukumbatia matumizi ya TEHAMA, na kila taasisi kutekeleza Dira 2050 kwa nafasi yake.
Maelekezo hayo yalitolewa katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha, Mkoani Pwani wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi za umma yalioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi.
Balozi Dk. Kusiluka alisema katika mwaka huu mpya wa fedha angependa kuona taasisi za umma zinaepuka matumizi yasiyo na tija, na kuelekeza fedha zaidi katika maeneo ya vipaumbele vya kitaifa kama vile miundombinu, afya, elimu, na huduma za kijamii.
“Watendaji Wakuu wanalo jukumu la kuhakikisha taasisi zao zinaendeshwa kwa misingi ya ufanisi na uwajibikaji mkubwa,” alisema Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa ufunguzi wa mafunzo yaliyowaleta pamoja wakuu wa taasisi za umma 114.
Balozi Dk. Kusiluka aliongeza kuwa ili taasisi za umma ziongeze ufanisi, zinapaswa kujenga uwezo wa ndani wa taasisi kwa kuboresha rasilimali watu, teknolojia na miundombinu.
Aidha, alizitaka taasisi za umma, kila moja kwa nafasi yake, kuhakikisha zinashiriki katika kufanikisha Dira 2050.
Dira hii inalenga kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu, yenye viwanda, mifumo ya kiutawala yenye uwazi, na ustawi kwa wananchi wote.
“Tunatarajia pato la Taifa kufikia $1 trilioni ifikapo 2050, huku pato la mtu mmoja mmoja likifia $7,000, hii sio kazi ndogo lakini tuna kila sababu ya kufikia lengo,” alisema Dk. Kusiluka.
Aliongeza: “Taasisi zetu ni nguzo muhimu ya utekelezaji wa Dira hii, na mafanikio ya Taifa letu yatategemea namna taasisi hizi zitakavyobadilika kifikra na kuendana na mahitaji ya mabadiliko ya kimkakati,” alisisitiza.
Aidha alisema mafunzo elekezi kwa wakuu wa taasisi za umma ni tukio muhimu ambalo linaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha utendaji kazi, uongozi bora na uwajibikaji katika sekta ya umma.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Mchechu, alisema anatarajia kuona taasisi za Umma zenye mwelekeo wa kibiashara zinaongeza ufanisi wa kiutendaji, mapato na faida, na hivyo kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali kuu.
“Taasisi hizi lazima ziendeshe shughuli zao kwa misingi ya kibiashara, zenye ushindani, ubunifu na tija ili kuchangia kikamilifu kwenye pato la taifa— kupitia gawio na michango mingine,” alisema Bw. Mchechu.
Hili, alisema, linakwenda sanjari na kukumbatia matumizi ya TEHAMA na hivyo taasisi za umma zinapaswa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya uwekezaji katika TEHAMA na kuhakikisha mifumo inasomana ili kuongeza ufanisi.
“Lazima tukumbatie matumizi ya TEHAMA kikamilifu ili kuleta tija iliyotarajiwa,” alisema Bw. Mchechu.
Aliongeza: “Mwisho wa siku tunataka kuona taasisi za umma zenye mrengo wa biashara, zinajiendesha kibiashara na hivyo kupunguza au kuondokana kabisa na utegemezi kutoka Serikali kuu.”
Kwa upande wa taasisi za huduma, Msajili wa Hazina alizitaka ziendelee kuboresha huduma zao kwa wananchi – kwa ubora, kwa wakati na kwa gharama nafuu.
“Huduma kwa umma si fadhila bali ni haki yao, na taasisi zetu ni lazima ziwahudumie kwa weledi na kujali mahitaji yao halisi,” alisema Bw. Mchechu.