Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amefanya ziara katika Makao Makuu ya Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo amepongeza juhudi za taasisi hiyo katika kuboresha afya na ustawi wa watu wa Afrika.
Akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dkt. Jean Kaseya, Waziri Kombo ameeleza kufurahishwa na kazi ya taasisi hiyo na kuitaja kuwa na heshima kubwa kimataifa, ingawa bado mataifa ya Afrika hayajaitumia ipasavyo. “Tunapaswa kuwa mabalozi wenu ili viongozi wetu waelewe kwa undani kazi mnayofanya,” alisema Mhe. Kombo.
Waziri Kombo amesisitiza kuwa kazi ya Africa CDC inagusa sekta za afya, elimu, michezo na utamaduni, na hivyo kuitaka taasisi hiyo kushirikiana zaidi na wizara mbalimbali za nchi wanachama huku akionesha utayari wa Serikali ya Tanzania kuimarisha uhusiano huo.
Aidha, Waziri Kombo amependekeza ushirikiano wa kiufundi kati ya Africa CDC na Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ambapo Tanzania imepanga kuanzisha vituo vya usambazaji wa dawa katika mipaka na wilaya zote. Pia amepongeza juhudi za Africa CDC katika kupambana na ugonjwa wa seli mundu, akieleza kuwa Tanzania iko tayari kushiriki kupitia mpango wa “Building a Better Tomorrow (BBT)” unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Dkt. Kaseya amempongeza Waziri Kombo kwa ziara hiyo na kusema kuwa Tanzania inaweza kuwa mshirika muhimu katika kusaidia Africa CDC kufikisha ujumbe wake kwa viongozi wa Afrika, hasa kwa kuzingatia nafasi ya Rais Samia kama Mwenyekiti wa sasa wa Chombo cha Usalama cha SADC.
Waziri Kombo pia ametembelea Kituo cha Dharura cha Uendeshaji kinachofuatilia zaidi ya matukio 140 ya kiafya barani Afrika, na kuelezwa jinsi taasisi hiyo inavyotumia teknolojia ya kisasa kulinda afya ya bara la Afrika.
Katika ziara hiyo, Mhe. Waziri Kombo aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo, pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda.