Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati aliposhiriki mjadala ya Wakuu wa Nchi na Serikali kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum-ACTIF 2025) kwenye kituo cha mikutano cha Radisson jijini St. George’s, nchini Grenada Julai 28.2025. Mheshimiwa Majaliwa anahudhuria jukwaa hilo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Jukwaa la Nne la Biashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (ACTIF) linapaswa kuja na majibu ya changamoto za kibiashara na uwekezaji zinazoyakabili mataifa ya Afrika na yale ya eneo la Karibiani.
Amesema kuwa changamoto hizo zinapaswa kujadiliwa kwa uwazi na kutaja bayana vikwazo vyote vinavyosababisha kutofanyika kwa biashara kati ya mataifa hayo.
Ameyasema hayo jana (Jumatatu, Julai 28, 2025) wakati akishiriki mjadala ya Wakuu wa Nchi na Serikali kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum-ACTIF 2025) linalofanyika katika kituo cha mikutano cha Radisson jijini St. George’s, nchini Grenada. Mheshimiwa Majaliwa anahudhuria jukwaa hilo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mbali ya kujadili changamoto hizo, nchi zetu zinapaswa kutengeneza mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye mataifa yetu. Kwetu sisi Tanzania, Aliko Dangote ni mfano hai, amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa kiwanda cha saruji.”
Viongozi wengine walioshiriki mjadala huo ni Waziri Mkuu wa Dominica, Roosevelt Skerritt; Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Amor Mottley; Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, Gaston A. Browne; Waziri Mkuu wa Saint Kitts and Nevis, Dkt. Terrance Drew; Waziri Mkuu wa St. Lucia, Philip J. Pierre pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Prudence Sebahizi.
ACTIF ilianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kiutamaduni baina ya mataifa ya Afrika na Karibiani. Katika kipindi cha miaka mitatu, jukwaa hilo limewezesha kuimarika kwa ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi, kusainiwa kwa hati za makubaliano na ushirikiano zenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni nne; hatua ambayo imechochea wazo la kuanzisha ukanda rasmi wa biashara kati ya nchi za Afrika na Karibiani.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Grenada, Dickon Thomas Mitchell alisema kuwa wanapaswa kurasimisha rasilimali na kuyapa nguvu majukwaa ya kiuchumi likiwemo hilo la Kibiashara na Uwekezaji baina ya Afrika na Karibiani. “Hatua hii itahakikisha vijana wetu wanatambua kuwa njia pekee ya nchi zetu kukua, inategemea maamuzi ya kiuchumi yanayofanywa sasa juu ya umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kwenye masuala ya kiuchumi na biashara baina ya Afrika na Diaspora.”
Naye, Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AFREXIMBANK, Prof. Benedict Oramah alisema kuwa jukwaa hilo linapaswa kuwa na taasisi zake ambazo zitakuwa na uwezo wa kuharakisha kuleta maendeleo.
“Kwa sasa, tunafanya kazi ya kuanzisha Benki ya Karibiani ambayo tunaamini itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa chachu ya kuwezesha ufanyaji biashara na kuendeleza viwanda kama AFREXIMBANK ilivyofanya barani Afrika.”
Madhumuni ya ACTIF ni kuimarisha mahusiano ya kihistoria na kiutamaduni baina ya Afrika na Karibiani; kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara na uwekezaji baina ya pande hizo mbili pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya pamoja.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Karibe, Marekani ya Kati na nchi za Venezuela na, Bw. Wilbroad Kayombo.