Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania pamoja na wataalamu wake waliotengeneza Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) wenye viwango vya kimataifa na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na bei za mifumo kama hiyo kwenye soko la kimataifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliyofanyika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Posta Jijini Dar es Salaam.
Amasema Benki Kuu ya Tanzania imekuwa taasisi ya kwanza Barani Afrika kuunda Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki ambapo jumla ya shilingi bilioni 81.32 zimeokolewa kwa kutumia wataalam wa ndani na kuongeza ufanisi wa Benki Kuu katika kusimamia ufanyikaji wa miamala pasipo vizuizi.
Aidha Makamu wa Rais ameigiza Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi husika, kama Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA) na Wizara zinazohusika, kuhakikisha wanasimamia vema Mfumo wa iCBS na mifumo mingine yote ya malipo, ili kuendelea kupata matokeo stahiki katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Aidha, amesisitiza zaidi kuhusu kujikita kwenye matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali katika kufanya miamala na malipo mbalimbali, ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa rai kwa Benki Kuu ya Tanzania kuhakikisha wanadhibiti na kuchukua hatua stahiki kwa wimbi la wakopeshaji kupitia mitandao ya simu na kuhakikisha wananchi hawaendelei kutapeliwa.
Aidha ameitaka Benki Kuu kuendelea kutoa elimu kwa Umma juu ya athari za kurubuniwa na matapeli hao na fursa sahihi za kupata mikopo nafuu katika Mabenki.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa wito wa kuhakikisha ulinzi wa hakimiliki ya Mfumo wa iCBS.
Aidha, ametoa wito kwa Wizara zote, kuongeza motisha kwa wabunifu wa ndani ambao wana mchango mkubwa katika kuokoa fedha za kigeni na kuongeza tija kwa ujumla.
Makamu wa Rais amesema Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua zaidi za kuimarisha mazingira ya utafiti na ubunifu ikiwa ni pamoja na kuongeza fedha za utafiti, kuanzisha vituo vingi vya ubunifu na vituo atamizi pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu, serikali, na sekta binafsi.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Emmanuel Tutuba amesema mfumo wa iCBS umesaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuleta maboresho makubwa kwenye maeneo mengi ikiwemo utoaji wa taarifa sahihi za serikali na kwa wakati, utoaji wa taarifa za miamala, ufungaji wa hesabu kwenye akaunti za wateja, upatikanaji wa taarifa kwa wafadhili, uhaulishaji wa fedha na ukokotoaji wa riba za kibenki.
Tutuba ameongeza kwamba uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika, thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika pamoja udhibiti wa mfumuko wa bei.
Amesema hadi kufikia Juni 2025 akiba ya fedha za kigeni ilifikia jumla ya dola za Marekani bilioni 6.2 ikiwa ni kiasi cha juu zaidi kufikiwa hapa nchini.
Amesema mara baada ya kufanya marekebisho ya sheria ya madini mwaka 2024 na kuiwezesha Benki Kuu kuanza ununuzi wa dhahabu kwa kutumia fedha za ndani, tayari Benki Kuu imenunua tani 6.6 za dhahabu safi zenye thamani ya dola za Marekani milioni 706.6 kiasi hicho cha dhahabu ni sawa na asilimia 110 ya lengo la kununua tani 6 kwa mwaka 2024/2025.
Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais pia amefunga rasmi Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania yenye lengo la kuonesha historia na maendeleo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) katika hafla iliyofanyika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Posta Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo maalum iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wauzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) katika hafla iliyofanyika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Posta Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo maalum iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania kwa Rais Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa uzinduzi wa MfumoMkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) katika hafla iliyofanyika Ofisi za Benki Kuu yaTanzania (BOT) Posta Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifungua rasmi Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania yenye lengo la kuoneshahistoria na maendeleo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Ufunguzi huo umefanyikawakati wa uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliyofanyika katikaOfisi za BOT, Posta Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai 2025.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa uzinduzi wa Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) uliyofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Posta Jijini Dar es Salaam leo tarehe 30 Julai 2025.