
Mbunge wa Bumbuli anayemaliza muda wake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), January Makamba, amesema amekubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM wa kuondoa jina lake katika mchakato wa kuwania tena ubunge wa Jimbo la Bumbuli.
Makamba ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Kamati Kuu ya CCM kutangaza majina ya wagombea ubunge kwa majimbo mbalimbali nchini, ambapo jina lake halikuwemo katika orodha hiyo ya awali.
“Kwenye CCM, dhana ya ‘kukatwa’ haipo. Ni aidha umependekezwa au umeteuliwa. ‘Kukatwa’ maana yake ni kwamba kuna nafasi unayostahili ambayo umeenguliwa, jambo ambalo si sahihi katika mfumo wetu,” alisema January Makamba.
“Wakati wa kuomba nafasi hizi, wote tunakuwa sawa – hakuna anayestahili zaidi ya mwingine. Kwa hiyo, hakuna dhana ya kukatwa. Ni aidha umependekezwa au hukupendekezwa; umeteuliwa au hukuteuliwa. Sisi hatukuteuliwa,” aliongeza Makamba.