
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ametangaza maandalizi ya mabasi takribani 100 kwa ajili ya kuwapeleka mashabiki katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kushuhudia na kushangilia mashindano ya CHAN.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Julai 30, jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha mashabiki wanapata fursa ya kuisapoti timu ya taifa katika mashindano hayo muhimu.
“Tumeshirikiana na wizara kuhakikisha mabasi ya kutosha yanapatikana. Wakuu wa wilaya wameshaelekezwa kuratibu usafiri huu kwa ufanisi, kutoka maeneo yote ya Dar es Salaam hadi uwanjani na kurudi,” alisema Chalamila.

Aidha, aliwahamasisha wafanyabiashara wadogo kuendelea na shughuli zao siku ya mashindano hayo, akisema kuwa fursa ya kiuchumi pia ipo wazi katika tukio hilo kubwa.
Mashindano ya CHAN yanatarajiwa kuibua msisimko mkubwa jijini Dar es Salaam, huku mkoa huo ukiwa mstari wa mbele katika maandalizi ya kuhakikisha mashabiki wanashiriki kwa wingi.